Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yaigeukia Namungo  

1c3f4283c4356b23f8cef2c8008f1a4d.jpeg Simba yaigeukia Namungo  

Sat, 29 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SIMBA leo itakuwa kwenye uwanja wa Majaliwa Lindi kucheza na Namungo ya huko katika mtiririko wa mechi za Ligi Kuu Bara.

Mechi hiyo ni kiporo kutokana na kushindwa kuchezwa kwa mujibu wa ratiba ya kawaida kwa vile timu hizo zilikuwa zikishiriki michuano ya kimataifa.

Simba ambao wapo kileleni mwa msimamo wa ligi wakiwa na pointi 61 baada ya kushuka uwanjani mara 25, watakuwa na kibarua kigumu ugenini dhidi ya Namungo ambao wanashika nafasi ya nane wakiwa na pointi 40 baada ya kucheza mechi 28.

Mara ya mwisho Simba kucheza Uwanja wa Majaliwa, ilikuwa msimu wa mwaka 2019/20 ambapo walibanwa mbavu na kulazimishwa suluhu katika mchezo waliotangaza ubingwa wa tatu mfululizo.

Akizungumza jana Kocha mkuu wa Simba, Didier Gomes, alisema anatarajia kukutana na upinzani mkubwa kutoka kwa wenyeji kwani kila timu inahitaji matokeo lakini wamejipanga kuondoka na pointi tatu katika mchezo huo.

“Mchezo huu una umuhimu mkubwa kwetu ukiangalia msimamo wa Ligi Kuu ulivyo hivi sasa timu tatu za juu zote zina nafasi ya kutwaa taji hivyo tunapaswa kupambana zaidi ili kupata matokeo tuzidi kusogea juu zaidi.

“Nimewaambia wachezaji wangu kuwa tunapaswa kuwa makini na kuongeza nguvu katika mapambano kuhakikisha tunarudi nyumbani na pointi tatu ili tuendelee kusalia juu ya msimamo wa ligi lakini nawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti,” alisema Gomes.

Naye Kocha Mkuu wa kikosi cha Namungo FC,Hemed Suleiman ‘Morocco’, alisema kuwa kupambana na kusaka pointi tatu wanajua haitakuwa mechi rahisi kwao lakini wamejipanga kuhakikisha wanashinda ili kuongeza hali ya kujiamini kikosini mwao.

“Tumefanya maandalizi ya kutosha naamini tutaenda kupata matokeo kutokana na morali iliyopo kikosini tumejipanga kuhakikisha pointi tatu zinabaki nyumbani ,” alisema Morocco.

Chanzo: www.habarileo.co.tz