Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yaichapa Mbeya City, yapaa kileleni

82816 Pic+simbAAA Simba yaichapa Mbeya City, yapaa kileleni

Tue, 5 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mshambuliaji Meddie Kagere amefunga bao lake la nane akiingoza Simba kuichakaza Mbeya City kwa mabao 4-0 katika mchezo Ligi Kuu Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mabao ya Simba yamefungwa na Kagere, Clatous Chama, Sharaf Shiboub na Deo Kanda na kuwafanya mabingwa hao kuendelea kujikita kileleni mwa Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 21.

Wakati Simba ikijikita kileleni mshambuliaji wake Kagere ambaye kabla ya mchezo wa leo alikuwa amecheza dakika 180, bila ya kufunga bao lolote na kuishuhudia Simba ikivuna pointi tatu katika mechi mbili dhidi ya Singida United na Mwadui.

Kagere alifunga bao lake kwa mkwaju wa penalti katika dakika 8, baada ya mshambuliaji Miraj Athumani kuangushwa katika eneo penalti.

Simba iliyoingia katika mchezo huo na mfumo wa 4-3-3 iliendelea kulisakama lango la Mbeya City katika dakika 42, kiungo Clatous Chama alifunga bao la pili kwa shuti kali akiwa nje ya eneo la 18 na kumwacha kipa wa Mbeya City hajui la kufanya na kuifanya Simba kwenda mapumziko wakiwa mbele.

Katika kipindi cha pili Simba iliendelea kulisakama lango la Mbeya City inayoundwa na vijana wengi huku wakionekana kuchoka kila muda unavyokwenda. Simba ilitumia nafasi hiyo katika dakika 78, kiungo Sharaf Shiboub alifunga bao lake la tatu msimu huu akimalizia vizuri krosi ya Chama aliyekuwa katika kiwango bora katika mchezo huo.

Winga Deo Kanda alifunga bao lake la kwanza tangu ajiunge na Simba akimtoka kipa Mbeya City, na kumalizia mpira wavuni na kuamsha shangwe kubwa kwa mashabiki mabingwa hao.

Ubao wazua jambo Uwanja wa Uhuru

Mashabiki wa Simba walianzisha wimbo wenye lengo la  kushinikiza bao lao la tatu liandikwe katika ubao wa matangazo.

Baada ya Shaaraf kuipatia Simba bao la tatu ni kama muandika matokeo katika ubao wa matangazo alitoka ndipo mashabiki hao walipostuka na kuanza kuimba  'huyupooo, oooh'.

Muitikio wake ulikuwa mkubwa kwa takribani dakika 10 ndipo shabiki mmoja wa Simba, akiwa amevalia jezi nyekundu, alipoenda katika ubao huo na kutoa kibao kilichokuwa kikionyesha wakiongoza mawili na kuweka tano.

Shangwe iliendeleea kuwa kubwa kwa mashabiki wa Simba dakika mbili baadae anayehusika na ubao wa matokeo uwanjani hapa, alistuka na kusogea haraka eneo hilo.

Wakati akisogea ndipo Simba, walipofunga bao la nne, kupitia kwa Deo Kanda, aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Ibrahim Ajibu.

Muweka matokeo katika ubao wa mtangazo alipanda haraka juu na kubadili kile kibao cha tano, kilichowekwa na shabiki wa Simba na kuweka cha 4-0.

Katika mchezo mingine jijini Tanga, wenyeji Coastal Union imekubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mbao.

Katika mchezo huo Mbao ilipata mabao yake kupitia Waziri Junior dakika ya 64 na Said Junior dakika ya 79, wakati Coastal ulipata bao dakika ya 16 kupitia kwa Shaaban Hamis.

Mtwara: Ndanda ikiwa nyumbani imeshinda 2-0 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Polisi Tanzania ilishinda bao 1-0 dhidi Alliance FC, huku JKT Tanzania ikiwa nyumbani ilikuba kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Tanzania Prisons.

Matokeo

Simba SC 4-0 Mbeya City

Coastal Union 1-2 Mbao FC.

JKT Tanzania 0-1 Prisons.

Polisi Tanzania 1-0 Alliance

Ndanda SC 2-0 Ruvu

Chanzo: mwananchi.co.tz