Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yaichapa Kagera Sugar yapaa kileleni

77632 Simbna+pic

Sat, 28 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mshambuliaji Meddie Kagere amefunga mabao mawili na kuiongoza Simba kurudi kileleni mwa Ligi Kuu Bara kwa kuifunga Kagera Sugar mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha pointi tisa (9), sawa na Kagera Sugar lakini wakitofautiana mabao ya kufunga.

Kagere mfungaji bora wa msimu uliopita ameendeleza makali yake ya kuzifumania baada ya kufunga bao dakika 4, na mkwaju wa penalti 78, pamoja na kutegeneza bao lililofungwa na beki Mohamed Hussen katika dakika 35.  

Katika mchezo huo, Simba walipata bao la mapema dakika ya nne baada ya Kagere kuunganishwa kwa kichwa krosi ya Deo Kanda kutoka mashariki mwa uwanja huo.

Nadhodha wa Kagera Sugar, Frank Kyaruzi aliyekuwa akicheza na Hassan Isihaka, alikuwa akionekana kutembea na Kagere, aliyekuwa akicheza peke yake kama mshambuliaji wa kati kiasili kwenye kikosi cha Simba.

Dakika ya 20, ambapo Sharaf Shiboub alikuwa akicheza kwenye eneo la kiungo, alipanda kwa haraka na kupiga shuti ambalo liliifanya Simba wapate kona, wakati ambao alikuwa akipanda na mpira, alionekana Kyaruzi kumzonga Kagere.

Pia Soma

Advertisement

Eneo lingine ambalo lilikuwa na ushindi kwenye dakika hizo 45 za kipindi cha kwanza ni kiungo ambalo kwenye kikosi cha Simba, walianza, Gerson Fraga, Deo Kanda, Mzamiru Yassin, Sharaf Shiboub na Ibrahim Ajibu.

Viungo hao, walikuwa na maelewano mazuri pindi wakiwa na mipira huku wakikutana na ushindani kutoka kwa Zawadi Mauya, Awesu Awesu na Ally Ramadhani wa Kagera Sugar.

Katika eneo hilo, ulikuwa ukichezwa mpira wa kasi na nguvu kutokana na aina ya wachezaji walioanza kwenye vikosi vya timu zote mbili. Ushindani mwingine ulionekana kwa Evarigestus Mujwahuki ambaye alikuwa akikutana na ushindani kutoka kwa Tairone Santos.

Ajibu ambaye alianza kwenye kikosi cha Simba kwa mara ya kwanza msimu huu, alikuwa na msaada mkubwa kwa Kagere kwenye safu ya ushambuliaji akitokea  winga ya kushoto huku Kanda akiwa kulia.

Dakika ya 26, mchezo huo, Ajibu alionyeshwa kadi  ya njano na mwamuzi, Emmanuel Mwandembwa  baada ya kushika mpira , Kagera Sugar walipata faulo hiyo karibu na eneo la hatari la Simba, ambapo Awesu Awesu, aliyekuwa msumbufu alishindwa kumfunga Manula kwa kupiga fyongo.

Dakika ya 29, Kagere alimanusra aifungie tena bao la pili Simba huku akiwa amezubaa, Kyaruzi na Isihaka alijiweka kwenye eneo zuri na kuitegea krosi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, lakini aliukosa mpira ule.

Akiwa amekabwa dakika ya 35, Kagera alileta madhara kwa Kagera Sugar, akiwa amelipa mgongo lango huku Tshabalala akipanda kwa kasi, walipasiana na beki huyo akapokea tena na kuifungia Simba bao la pili kwenye mchezo huo.

Shughuli ya Kagere kwa Kyaruzi ilimfanya mwishoni mwa kipindi cha kwanza kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime kumnyenyua mzoefu Juma Nyoso aanze kupasha.

Kabla ya kumalizika kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza, mpira ulisimama kwa dakika moja na nusu,  kutokana na vurugu za hapa na pale kwa wachezaji baada ya kufanyiwa madhambi, Ajibu na Zawadi Mauya.

Mwanzoni mwa kipindi cha pili, Maxime alifanya mabadiliko kwenye kikosi chake kwa kumtoa Kyaruzi aliyezidiwa na Kagere mwishoni mwa kipindi cha kwanza na kuingia Nyoso.

Maxime alifanya mabadiliko mengine kwa kumuingiza Peter Mwalyanzi, aliyechukua nafasi ya Mhilu, aliyeshindwa kufua dafu mbele ya Tshabalala huku kocha wa Simba naye akifanya mabadiliko ya kuingia kwa Miraj Athuman na kutoka Kanda.

Dakika 77 Miraj Athuman alifanyiwa madhambi ndani ya 18 na beki wa Kagera Sugar, Zawad Mauya na penalti hiyo ilipigwa na Kagere ambaye aliiweka moja kwa moja wavuni na kufanya Simba waongoze kwa magoli 3-0.

Mbrazil Wilker Da Silva aliingia dakika ya 88 huku Kagere akipumzishwa na kucheza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara ambao Simba ilivunja mwiko wa msimu uliopita ambapo walipoteza kwenye uwanja huo dhidi ya Kagera Sugar kwa  mabao 2-1.

Ushindi wa mabao 3-0 ambao Simba waliupata dhidi ya Kagera Sugar ni ushindi mkubwa zaidi kuupata kwenye uwanja  wa Kaitaba, mwaka jana, waliwahi kuwafunga mabao 2-0.

REKODI ZAO

Rekodi zinaonyesha ndani ya misimu sita, Kagera Sugar na Simba wamekuta mara 11.

Rekodi ya msimu uliopita Simba walikubali kulala mechi zote mbili kwa maana ya kufungwa ugenini mabao 2-1, na kufungwa tena nyumbani kwao uwanja wa Uhuru bao 1-0, ambalo alijifunga beki wa kushoto Mohammed Hussen 'Tshabalala'.

Msimu 2017-18, mchezo wa kwanza Simba walishinda mabao 2-0, ambayo yalifungwa na John Bocco pamoja na Said Ndemla, wakati mechi ya marudiano Simba wakiwa ni siku yao ya kukabidhiwa ubingwa wa ligi mbele ya Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, walifungwa bao 1-0, ambalo liliwekwa kambani na Edward Cristopher.

Msimu 2016-17, mechi yaa kwanza Simba wakiwaa nyumbani walishinda mabao 2-0, wakati ule wa marudiano Kagera wakiwa katika uwanja wa Kaitaba walishinda mabao 2-1.

Msimu 2015-16, mchezo wa kwanza Simba walishinda mabao 3-1, kama ambavyo walishinda tena mechi ya marudiano bao 1-0. Msimu wa 2014-15, mechi ya kwanza Kagera walifungwa bao 1-0, kama ambavyo ilikuwa katika mechi ya pili kwa kufungwa tena mabao 2-1.

Rekodi zinaonesha kuwa katika misimu mitano wamekutana mara kumi, huku Simba akiondoka na ushinda katika michezo mitano kama ambavyo ilivyo kwa wapinzani wao Kagera Sugar na hakuna mchezo ambao ulimalizika kwa sare ya aina yoyote ile.

Simba wameweza kufunga mabao 15 na wao wakiruhusu nyavu zao kutikiswa kwa kufungwa mabao tisa.

Vikosi

Kagera Sugar: Said Kipao, Mwaita Gereza, David Luhende, Hassan Isihaka, Frank Kyaruzi, Zawadi Mauya, Awesu Awesu, Ally Ramadhani,  Evarigestus  Mujwahuki, Abdallah Seseme, Yussuf Mhilu.

Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Tairone Santos, Pascal Wawa, Gerson Fraga, Deo Kanda, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Sharaf Shiboub na Ibrahim  Ajibu.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz