Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yagawanyika vipande viwili

65717 Pic+simba

Sat, 6 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ ametishia kujitoa Msimbazi ikidaiwa hayupo tayari kufanya kazi na mwenyekiti wa klabu hiyo, Sued Mkwabi.

Kutokana na mvutano huo ambao umedumu kwa zaidi ya miezi miwili, inadaiwa kuwa Mo Dewji amewaambia baadhi ya wajumbe wa bodi ya klabu hiyo kuwa Mkwabi amekuwa ‘akimuhujumu’.

Habari kutoka klabu hiyo, zinadai kuwa Mkwabi amekuwa akiwashutumu baadhi ya wajumbe walioteuliwa na Dewji, jambo ambalo mwekezaji huyo anaona ni hujuma kwake.

Habari hizo zinasema Dewji amekuwa akilalamika kuwa Mkwabi amekuwa akichelewesha baadhi ya majukumu anayopewa, ikidaiwa hata hati ya kiwanja inayoshikiliwa na Hamisi Kilomoni anahusika.

Alipotafutwa Mkwabi ili kutoa ufafanuzi juu ya taarifa hizo alisema, “nipo safarini nje ya nchi, hivyo sielewi mambo yanayoendelea huko, nashindwa kujibu mambo ambayo siyafahamu kama kuna lolote basi kuna viongozi huko wanaoweza kusaidia kutoa ufafanuzi ila nafahamu ndani ya Simba hakukuwa na tatizo lolote.”

Mvutano huo ulishika kasi Mei 30 mwaka huu wakati wa Mo Simba Awards, baada ya Mkwabi kutopewa nafasi ya kuzungumza kwa nafasi yake ya mwenyekiti badala yake nafasi hiyo alipewa Salim Abdallah ‘Try Again’.

Pia Soma

Inadaiwa kuwa Mkwabi amekuwa akiona kama madaraka yake Simba yanaporwa na kwamba hana nguvu tofauti na alivyotarajia.

Inadaiwa kuwa kutokana na hilo Mkwabi amekuwa akihoji mara kwa mara kuhusu uwezekaji wa Sh20 bilioni, na licha ya kupewa majibu amekuwa akirudia mara kwa mara kuhoji jambo hilo.

Kutokana na msuguano huo, inadaiwa kuwa ili hali itengamae Msimbazi mmoja kati ya wenyeviti hao, Dewji au Mkwabi anapaswa kukaa pembeni na ndio maana mwekezaji huyo anahisi ni nafasi nzuri kwake kuondoka.

Tetesi za kujiengua kwa Dewji (44) ambaye Desemba 3, 2017 alitangazwa kuwa mwekezaji wa klabu hiyo kwa hisa za asilimia 49, zilianza kuzagaa tangu mwezi uliopita, lakini wiki hii mvutano huo ulizidi zaidi.

Ili kuokoa jahazi hilo, mawaziri kadhaa wa Serikali wamekutana na Dewji kwa ajili ya kumtuliza, lakini inadaiwa kuwa bado kuna shinikizo kubwa la kumtaka Mkwabi ajiuzulu au yeye kuondoka.

Kuthibitisha kuwa mambo hayajatulia Msimbazi, Dewji jana aliandika katika kurasa zake za mitandao ya kijamii ya Instagram na Twitter kwamba, “watu wenye nia mbaya. Kazi yao sio kujenga, ni kuvunja tu. Kaa nao mbali. Narudia kaa nao mbali sana”.

Hata hivyo, ujumbe wa tajiri huyo nchini ulibeba maswali mengi ambayo hayakupatiwa ufumbuzi kwani, hata wajumbe wa bodi ya klabu hiyo walipohojiwa walionekana kuwa wazito, lakini wakasisitiza kuwa hayo ni mambo ya ndani ambayo hayapaswi kutoka nje.

“Unajua Simba ni taasisi, kuna mambo mengi yanaendelea ambayo ni makubwa na madogo, hivyo sio busara kuanza kuyazungumza hayo kwa sasa, tusubiri kuna viongozi wa juu ambao wanaweza kutolea ufafanuzi kama kuna tatizo ndani ya bodi,” alisema mjumbe mmoja wa Simba.

“Kukwaruzana na kutokuwa na mahusiano mazuri sehemu yoyote ile ya kazi kupo ingawa inategemea na nini kinasababisha hali hiyo, hivyo tusubiri huenda akawa Mo mwenyewe wa kutolea ufafanuzi juu ya taarifa hizo zinazomuhusu au mwenyekiti wa klabu, Sued Mkwabi,” alisema mjumbe huyo.

Mjumbe mwingine alisema “Wengi wanajiuliza nini kimetokea ila kuna baadhi ya wajumbe nadhani wanashindwa kuelewa maana ya uwekezaji ila nadhani mambo yatakaa sawa tu.”

Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori alipotafutwa simu yake iliita bila kupokewa, lakini jioni alionekana katika picha akimsainisha mchezaji wa Gor Mahia ya Kenya, Francis Kahata.

Chanzo: mwananchi.co.tz