Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yaficha straika hotelini Dar

Kibu Pi Data Simba yaficha straika hotelini Dar

Fri, 9 Jul 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kocha wa Simba, Didier Gomes amewaambia viongozi kwamba ; “Iwe iwavyo namtaka yule rasta wa Mbeya City hapa.” Kocha huyo anamaanisha wanase saini ya straika Kibu Denis ambaye watani zao Yanga nao wanamfikiria.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata ndani ya Simba ni kwamba, Gomes ameonyesha mapenzi ya wazi na mchezaji huyo na akawasisitiza viongozi wafanye juu chini asaini Simba .

Amewaambia kwamba katika wachezaji wote wazawa aliowaona kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, Kibu ndiye straika pekee ambaye anaweza kuwa mbadala wa Meddie Kagere kwenye kikosi chake cha kwanza pale atakapoamua kuanzisha straika mmoja,wawili au watatu. Simba kusikia hivyo fasta wakamvutia waya mchezaji huyo na juzi Jumatatu akatua Dar es Salaam na wakamficha sehemu ambayo Yanga hawawezi kumuona kumshawishi. Simba muda wowote kuanzia leo matajiri wa Msimbazi wakiongozwa na Mohammed Dewji ‘Mo’ watamsainisha Kibu ambaye amekuwa machacchari mpaka Taifa Stars.

Mwanaspoti linafahamu kwamba Yanga wanamfikiria Kibu lakini huenda ikawachukua muda kumsainisha kwavile Kocha Nabi Nasreddin amesisitiza kabla mchezaji yoyote hajapewa mkataba lazima wamjadili kwa kina.

Baada ya kufika Dar, Kibu amefichwa katika moja ya hoteli ambayo Simba wote wamekula kiapo mpaka na mchezaji kwamba asiseme.

Mabingwa hao watetezi wa ligi kama watakubaliana kumsainisha (Kibu), maana yake atakuwa mchezaji wa pili mzawa baada ya awali kuanza na kipa wa Tanzania Prisons, Jeremia Kisubi.

Habari zinasema Gomes, tayari amewaambia amevutiwa kwa kiasi kikubwa na Kibu kwani amekuwa akieleza sifa nyingi ambazo mchezaji huyo anazo na zile atakazokuja kumuongezea ili kuwa mchezaji bora zaidi.

“Amesema Kibu anaweza kufanya kazi kama zile ambazo Meddie Kagere, amekuwa akizifanya katika kila mechi ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” alisema. “Alituambia Kibu anaweza kusaka mipira eneo lote la mbele na akatengeneza nafasi kwa mchezaji mwingine kufunga jambo ambalo litawafanya kina Clatous Chama, Luis Miquissone, Chriss Mugalu, John Bocco na wengine kucheza kwa uhuru, pia anaweza kufunga,” alisema kigogo huyo.

Alipoulizwa Gomes mwenyewe kuhusiana na usajili licha ya kukiri kuvutia na baadhi ya wachezaji kwenye timu nyingine za ligi lakini akasema kwa sasa anachokiangalia zaidi ni kumaliza vizuri mechi zilizobaki za ligi na Kombe la Shirikisho la Azam ( ASFC ) watakutana na Yanga Julai 25 mkoani Kigoma.

“Tutafanya usajili wa wachezaji bora, kulingana na mahitaji na mapungufu ya timu ambayo tumeyaonyesha msimu huu katika mashindano yote.Tusubiri kwanza muda ufike ndio tutaeleza kila kitu,” alisema.

Kwa upande wa Kibu, alikiri kuwa amefanya mazungumzo na uongozi wa Simba ila hawezi kuweka wazi kwamba amemalizana nao au bado.

Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe alisema; “Akili yetu haipo kwa Kibu, kwani nguvu tumewekeza katika mechi zetu mbili ngumu ambazo tumebaki nazo kwani tumepanga kushinda kusalia katika ligi.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz