MSHAURI wa Mwekezaji wa Klabu ya Simba, Crescentius Magori, ameanika siri ya ushindi wa mabao 2-0, kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana na kuwataka wanachama na mashabiki wao kupuuza maneno ya baadhi ya watu kuwa ilikutana na timu mchekea.
Akizungumza baada ya kuwasili nchini wakitokea jijini Gaborone, Botswana juzi, Magori ambaye ni mshauri wa Mohamed Dewji, mwekezaji wa klabu hiyo, alisema Simba imepata matokeo mazuri kutokana ukweli kwamba kwa sasa wana uzoefu na michuano hiyo mikubwa ndani na nje ya uwanja, vinginevyo hali ingekuwa ngumu.
"Tulijiandaa na mechi ngumu. Na hii ni kwa sababu hivi sasa sisi ni wazoefu wa mashindano haya, haikuwa rahisi hata kidogo kama watu wanavyosema. Hii timu si mchekea kama watu wanavyodai, hivi majuzi kabla ya kucheza mechi yetu walicheza michezo miwili Afrika Kusini, wakatoka sare dhidi ya Mamelodi Sundowns na kufungwa bao 1-0 dhidi ya Orlando Pirates.
"Ni timu inayomilikiwa na kampuni ya mgodi wa almasi, wamesajili wachezaji wazuri, saba wanacheza timu ya Taifa ya Botswana na watatu ni wachezaji wa kigeni kutoka Afrika Kusini, kwa hiyo siyo timu ya mchezo mchezo," alisema Magori.
Alisema kilichotokea ni kwamba kwa sasa Simba ina wachezaji wazuri wenye uzoefu na ukomavu kwenye michezo ya kimataifa wakicheza ndani na nje ya nchi, lakini wao kama viongozi na makocha walijipanga madhubuti.
"Kocha aliisoma timu, tukapata mabao mawili ya haraka, alipanga mipango yake mizuri akalinda hadi mwisho. Mambo ya figisu huwa yanapunguzwa kama viongozi mkijipanga vizuri. Kuna watu walitangulia kwa ajili ya kuweka mambo sana. Na sisi pia tukafuata kabla timu haijawasili. Hii inaonyesha ni jinsi gani tulivyojipanga kukabiliana na mechi ngumu za kimataifa kama hizo," alisema.
Magori aliwataka wanachama na mashabiki wa Simba kujitokeza kwa ajili ya kuishangilia timu hiyo Jumapili wakati wa mechi ya marudiano, Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambayo wameruhusiwa kuingiza watazamaji 15,000 tu.