Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba waoga noti

33405 Pic+simba Tanzania Web Photo

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Uongozi wa klabu ya Simba umewamwagia wachezaji wake noti ikiwa ni pongeza na motisha kwa kuitoa Nkana Red Devils ya Zambia, mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Abdallah Salim ‘Try Again’ alisema jana kuwa wote walioanza walizawadiwa Sh4mil kila mmoja wakati waliokuwa benchi walipata Sh2mil kila mmoja.

Alisema kuwa fedha hizo ni mwanzo kwani wakizidi kufanya vizuri zaidi mbele ya safari wataoga noti kila wakati.

Simba iliitoa Nkana Red Devils kwa jumla ya mabao 4-3, mchezo wa kwanza Simba ilipoteza kwa mabao 2-1 lakini juzi iliivimbia na kuipiga 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa.

Mabingwa hao wa soka Tanzania wanasubiri Shirikisho la Soka Afrika, (CAF) kupanga droo ya makundi Desemba 28 huko Cairo, Misri.

Mbali na Simba, timu nyingine zilifuzu makundi ni TP Mazembe, AS Vita (DR Congo), Esperance na Club Africain (Tunisia), Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates (Afrika Kusini), Al-Ahly na Ismaily (Misri), CS Constantine na JS Saoura za Algeria.

Nyingine ni Horoya (Guinea), Wydad Casablanca (Morocco), Lobi Stars (Nigeria), Asec Mimosas (Ivory Coast) na FC Platinum ya Zimbabwe.

Kwa kufuzu hatua hiyo ya makundi, Simba imejihakikishia kiasi cha Dola 550,000 (zaidi ya Shilingi 1.2 bilioni) ambazo zinaweza kuongezeka zaidi endapo wataingia robo fainali, nusu fainali au kutwaa ubingwa.

Akizungumzia mchezo huo, Try Again alisema: “Tunamshukuru Mungu tumeingia hatua ya makundi. Sisi kama uongozi tutakutana na kupanga mikakati ya kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye hatua hiyo.

“Zipo kasoro kadhaa ambazo timu imezionyesha dhidi ya Nkana lakini hilo ni jukumu la kocha. Kuna maeneo ambayo yanatakiwa kuimarishwa na jukumu hilo tumemuachia kocha mkuu. Kama ataona inafaa kuongeza nguvu kwenye baadhi ya maeneo tutafanya hivyo.

“Tunafahamu hatua inayokuja ni ngumu hivyo kama uongozi tutakutana ili kupanga mikakati ya kufanya vizuri kwa sababu hatua tunayoenda ni ngumu na kama hukujipanga vizuri, uwezekano wa kufanikiwa ni mdogo,” alisema mjumbe huyo wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, SalIM Abdallah ‘Try Again’

Hata hivyo wakati Try Again akianika mipango ya Simba kulekea hatua ya makundi, wadau wa klabu hiyo wameiuma sikio kwa kuipa ushauri wa nini inapaswa ikifanye ili iweze kufanya vizuri.

Wadau walonga

“Kuna haja ya kutafutwa mwanasaikolojia wa kuwajenga wachezaji kisaikolojia ili waweze kujua thamani yao inaenda kupambanishwa na viwango vya juu pia washirikiane na wachezaji wa zamani kushauriana ama wapate muda wa kuwajenga wachezaji,”alisema Kocha na mchezaji gwiji wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni.

Beki wa zamani wa Simba ambaye alikuwemo kwenye kikosi kilichofuzu hatua ya makundi mwaka 2003, Boniface Pawasa amewataka wachezaji wa timu hiyo kutobweteka na ushindi walioupata.

Kikubwa wanapoingia hatua ya makundi, waamini wanaweza wakafika mbali zaidi. Wasijenge akili zao kwamba ndio mwisho. Kikosi ni kizuri na kinaweza kufanya maajabu,” alisema Pawasa.

Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Mzee Hassan Dalali, ameitaka timu yake kuongeza umakini kwenye hatua ya makundi ili iweze kufanya vizuri.

“Hatua hiyo tunayoenda ni ngumu sana hivyo nawaomba wachezaji wetu wajitume na wawe na umakini wa hali ya juu, hapo naamini tutafika mbali na ikiwezekana hata kutwaa ubingwa. Tunaweka rekodi ya kushindana kimataifa na nchi nyingine, hilo ni jambo la kujivunia,” alisema Dalali.



Chanzo: mwananchi.co.tz