Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba mdomoni mwa Singida United

81895 Pic+simba Simba mdomoni mwa Singida United

Mon, 28 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/mikoani. Mtifuano wa Ligi Kuu Tanzania unaendelea leo katika viwanja mbalimbali ambapo mechi sita zinatarajiwa kupigwa, huku mabingwa watetezi Simba wakiikabili Singida United kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.

Katika Uwanja wa Mabatini - Kibaha mkoani Pwani Ruvu Shooting wataikaribisha Azam FC, JKT Tanzania watakuwa ugenini kucheza na Mwadui FC kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Mbao FC itacheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Lipuli na Coastal Union watakuwa mjini Iringa huku Biashara United ikiikaribisha Namungo mjini Musoma.

Simba inaingia katika mchezo wao na Singida huku ikijivunia rekodi bora dhidi ya wapinzani wao hao kwani katika mechi nne walizokutana wameshinda zote. Tangu ipande Ligi Kuu 2017, Singida United imekutana na Simba mara nne na kufungwa mabao 10, huku ikishindwa kutikisa nyavu za wapinzani wao hata mara moja. Hata hivyo, timu hiyo ilifungana bao 1-1 na Simba kwenye mchezo wa Kombe la Kagame uliopigwa Julai 11, 2018 jijini Dar es Salaam.

Kwa mara ya kwanza Simba na Singida United walikutana kwenye Ligi Kuu Januari 18, 2018, na walishinda mabao 4-0 yaliyofungwa na Shiza Kichuya, Asante Kwasi na Emmanuel Okwi ambao kwa sasa wote hawapo katika kikosi hicho. Mechi ya pili ilichezwa Mei 12, 2018 kwenye Uwanja wa Namfua, Singida na Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Shomary Kapombe.

Katika msimu wa 2018/2019, Desemba 29, mwaka jana, Simba ilishinda kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na John Bocco ambaye ataukosa mchezo wa leo kwa kuwa hayupo fiti akiwa ametoka kuuguza majeraha pamoja na Kichuya.

Mechi ya mzunguko wa pili ilifanyika Mei 21 kwenye Uwanja wa Namfua na Simba ilishinda 2-0 yaliyofungwa na Meddie Kagere.

Pia Soma

Advertisement
Katika msimamo wa ligi hiyo, Simba inaongoza ikiwa na pointi 15 kutokana na mechi tano ilizoshinda ilhali Singida United iko mkiani na pointi tatu katika mechi saba ilizoshuka uwanjani.

Kauli za makocha

Kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema licha ya Singida United kutokuwa na matokeo mazuri, lakini wanategemea ushindani kutoka kwao katika mchezo huo. “Mazingira ya uwanja tunaoutumia katika mchezo huu siyo rafiki sana, lakini tumejipanga kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa,” alisema.

Hata hivyo, licha ya kocha wa Singida United, Ramadhan Nswanzurwimo kutopatikana jana kuzungumzia mchezo huo, mkurugenzi wa timu hiyo, Festo Sanga alisema benchi la ufundi linatambua ukubwa wa timu ya Simba katika soka la Tanzania, lakini limeahidi kupambana ili wapate ushindi utakaowabeba kujinasua kutoka mkiani.

Imeandikwa na Thobias Sebastian na Bertha Ismail

Chanzo: mwananchi.co.tz