MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wamezidi kukaribia ubingwa baada ya kuifunga Polisi Tanzania bao 1-0 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza jana.
Kabla ya kuanza mchezo huo timu zote na mashabiki walisimama kwa dakika moja kumkumbuka Rais wa kwanza wa Zambia, Kenneth Kaunda ambaye alifariki Alhamisi iliyopita.
Katika mchezo huo Simba ilijipatia bao dakika ya 26 lililofungwa na Luis Miquissone kwa mpira ya faulo uliomshinda kipa wa Polisi Mohamed Yusuf baada ya Shomari Kapombe kuchezewa faulo.
Huu ni mchezo wa pili Simba kuifunga Polisi msimu huu kwani katika mchezo wa kwanza walipokutana Uwanja wa Benjamin Mkapa, walishinda mabao 2-0.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani kila mmoja alishambulia lango la mpinzani wake kwa zamu na kuifanya Simba kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kila timu ilizidisha mashambulizi baada ya kufanya mabadiliko kadhaa na dakika ya 72 Aishi Manula aliokoa kichwa cha Gerald Mdamu aliyeingia kipindi cha pili.
Wachezaji wa Polisi, Pato Ngonyani, Hassan Nassoro, Tariq Seif na Abdulaziz Makame waliingia mara kadhaa katika lango la Simba lakini mashuti yao yaliokolewa na Manula na mengine kwenda nje.
Kwa matokeo hayo Simba inaendelea kuwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 70 baada ya kucheza michezo 28 na Polisi Tanzania wanabaki katika nafasi ya nane wakiwa na pointi 41 baada ya kucheza michezo 31.
Simba wanatarajia kucheza na Mbeya City katika Uwanja wa Benjamin Mkapa keshokutwa na baada ya hapo Juni 26 watacheza mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Azam FC, Uwanja wa Majimaji, Songea.