Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba kuwakabili  Dodoma Jiji leo 

D8ad10aa2ef038fc46b77d03414e857d.jpeg Simba kuwakabili  Dodoma Jiji leo 

Tue, 27 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wanashuka dimbani kuwakabili Dodoma Jiji kutoka Makao Makuu ya nchi Dodoma, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam leo.

Simba ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 58 baada ya kushuka uwanjani mara 24, huku mpinzani wake Dodoma Jiji ikishika nafasi ya sita katika msimamo ikiwa na pointi 38 baada ya michezo 27.

Wekundu wa Msimbazi wanaingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu nzuri dhidi ya Dodoma Jiji, ambapo katika mchezo wa kwanza waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mtanange uliochezwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Akizungumza jana, Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes alisema kikosi chake kinaendelea vizuri na vijana wake wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo ambao ni muhimu kwao kuendeleza wimbi la ushindi na kuzidi kujikita kileleni mwa msimamo.

“Malengo yetu ni ubingwa, ili tuweze kufanikisha tunapaswa kushinda kila mchezo ulio mbele yetu ili kujiweka katika mazingira mazuri.”

“Tulikuwa na ratiba ngumu michezo mitatu mfululizo tumecheza ugenini, sasa tumerejea nyumbani nawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti,” alisema Gomes.

Naye Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Vicent Barnabas alisema wataingia uwanjani kupambana na kusaka pointi tatu ingawa wanajua haitakuwa mechi rahisi kwao lakini wamejipanga kuhakikisha wanashinda ili kuongeza morali katika harakati za kusaka upenyo wa kuingia nafasi ya nne.

“Tumefanya maandalizi ya kutosha, naamini tutaenda kupata matokeo mazuri kutokana na morali iliyopo kikosini, tumetoka kupata sare nyumbani ambayo iliharibu hesabu zetu hivyo tumejipanga kuhakikisha tunaondoka na pointi tatu,” alisema Makata.

Michezo mwingine wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa leo ni Gwambina watakuwa nyumbani kuwakaribisha Mwadui FC wanaoshika mkia katika msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 18.

Chanzo: www.habarileo.co.tz