Dar es Salaam. Uongozi w Simba umethibitisha utacheza mechi tatu za kirafiki dhidi ya Bandari FC ya Kenya, Aigle Noir ya Burundi pamoja na Mashujaa ya Kigoma kabla ya kukutana na Azam FC Oktoba 23.
Taarifa hiyo imethibisha na uongozi wa Simba leo kuwa katika mapumziko ya wiki mbili kupisha michezo ya kirafiki ya Kimataifa kwa timu za Taifa katika Kalenda Shirikisho la Soka Duniani Fifa wekundu hao watakuwa na mchezo wa kwanza dhidi ya Bandari ya Kenya.
Bandari inayoshiriki Ligi Kuu Kenya kwa sasa ndio wawakilishi wa Kenya katika Kombe la Shirikisho Afrika ambapo watakutana na Simba Oktoba 12.
Baada ya mchezo huo Simba itasafiri kwenda Mkoani Kigoma kucheza mechi zingine mbili ambapo Oktoba 14 itakutana na Mashujaa FC katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Ziwa Tanganyika.
Mchezo wa mwisho kwa Simba utakuwa Oktoba 16 watakapokutana na Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Burundi, Aigle Noir utakaopigwa katika uwanja huhuo.
Tayari muandaaji wa mechi hizo mbili za Mkoani Kigoma, Othman Kaumo amesema maandalizi ya kuwapokea vinara hao wa Ligi Kuu Bara na Mabingwa watetezi yanaendelea kwa kasi huku muamko mkubwa ikiwa ni mashabiki kuanza kuulizia tiketi za mechi hizo mbili.
Benchi la ufundi la Simba chini ya kocha Patrick Aussems katika kujiandaa na mchezo wa Azam FC utakaopigwa Oktoba 23, kwenye Uwanja wa Uhuru walihitaji mechi hizo kujiandaa na mchezo huo mgumu.