Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba kuikabili Coastal

36c81689021bcbc42a6da107cabef472.jpeg Simba kuikabili Coastal

Thu, 23 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MICHEZO mitano ya raundi ya 37 ya Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo kwenye viwanja tofauti, huku mabingwa wa tetezi, Simba watakuwa ugenini kuwakabili Coastal Union, mechi itakayofanyika katika dimba la Mkwakwani jijini Tanga.

Simba wanaingia kwenye mchezo huo wakisaka ushindi ili kuongeza ari ya wachezaji wa kikosi hicho kujiaandaa na mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) uliopangwa kuchezwa Agosti 2 dhidi ya Namungo FC kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga.

Wapinzani wao, Coastal Union wenyewe ni kama wanataka heshima kwa mashabiki wao kwani hawana chakupoteza kutokana na nafasi waliyopo katika msimamo wa ligi hiyo. Simba wanaoongoza ligi kwa pointi 84, wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kutoka kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Alliance wakati Coastal wana pointi 52 wakiwa katika nafasi ya sita.

Rekodi za mechi ya mzunguko wa kwanza, Simba waliibuka na ushindi wa mabao 2-0, hivyo Coastal leo hawatakubali kupoteza mchezo huo kirahisi zaidi ya kupania kulipa kisasi baada ya kufungwa mchezo wa awali.

Kuelekea kwenye mchezo huo, kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola alisema bado wanahitaji kuendeleza ushindi kwenye mchezo huo ili kuwapa burudani mashabiki wa timu hiyo, hususani wanaoishi Tanga kwa kuwaunga mkono.

Alisema katika mchezo huo, maandalizi yote yamekamilika na wachezaji wote wamepewa malengo ya kutimiza wajibu wao wakiwa uwanjani ili kuendelea kutunza heshima kwa taji walilokwishatwaa. Kwa upande wake, Kocha wa Coastal, Juma Mgunda alisema michezo yote iliyobaki ni ya kukamilisha ratiba lakini watapambana kuhakikisha wanalinda heshima yao.

“Michezo yote iliyosalia tunahitaji ushindi ili kusaka heshima kwa mashabiki wa timu yetu kwa kutuunga mkono kwenye kipindi chote cha msimu tangu ulipoanza,” alisema Mgunda.

Katika michezo mingine leo, Azam FC watawakaribisha Mbeya City mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Chamazi wakati huo, Polisi Tanzania watakuwa kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi kuikabili JKT Tanzania.

Michezo mingine, Lipuli watakuwa kwenye uwanja wao wa Samora kuwakaribisha Ruvu Shooting na Alliance watakuwa kwenye dimba la Nyamagana, Mwanza wakicheza dhidi ya Ndanda FC.

Chanzo: habarileo.co.tz