Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

`Simba kufanya maajabu’

03e3394ed9976213f4658a7e06f6bd64.jpeg `Simba kufanya maajabu’

Sat, 22 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KOCHA Mkuu wa timu ya Simba, Didier Gomes amesema kuwa leo watawafurahisha mashabiki wao kwa kulipa kisasi na kurudisha heshima kwa kuhakikisha wanashinda na kuingia hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba wanaingia katika mchezo huu wakiwa nyuma kwa mabao 4-0 waliyopoteza mbele ya Kaizer Chiefs katika mchezo wa kwanza wa robo fainali, mtanange uliochezwa katika Uwanja wa FNB jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Gomes, alisema kuwa mchezo uliopita walimiliki mpira sana wakapiga pasi zaidi ya 600, kesho watacheza soka la kushambulia zaidi ili kuweza kutengeneza nafasi nyingi za kufunga ili kupata mabao zaidi ya manne.

“Nina furaha na kile kilichokuwa kinatokea katika uwanja wa mazoezi, wachezaji wangu walikuwa wanapambana sana kila mmoja akinionesha kuwa yuko tayari kwaajili ya mchezo huu najua Kaizer Chiefs ni wazuri katika kuzuia, lakini tumelifanyia kazi suala hili.

“Mpira ni vita, lakini tutacheza kiungwana tutakuwa makini na washambuliaji wawili wa kati wa Kaizer Chiefs, Samir Nurkovic na David Castro ni wachezaji wenye uwezo mzuri wanaotoa upinzani ,” alisema Gomes.

Alisema kuwa wachezaji wake wamepanga kwenda kufanya miujiza katika mchezo huo na kuilinda heshima ya Simba, kwani wiki hii katika uwanja wa mazoezi walikuwa wakijiapiza kuwa wanaenda kufanya maajabu.

Naye Kocha Mkuu wa Kaizer Chiefs, Gavin Hunt alisema kuwa anaamini utakuwa mchezo mgumu licha ya kuibuka na ushindi mkubwa katika mtanange wa kwanza, bado hawaamini kama tayari wamefuzu hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Naamini utakuwa mchezo wenye upinzani mkubwa tumekuja kupambana ili tuweze kupata matokeo na kusonga mbele, wachezaji wote waliokuja wako fiti hakuna ambaye ana maumivu wala adhabu,” alisema Hunt.

Mwaka 1979, Simba ilifanya maajabu baada ya kufungwa mabao 4-0 na Mufulira Wanderers ya Zambia katika mchezo wa Klabu Bingwa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) kabla ya kuipindua matokeo kwa kushinda 5-0 Zambia na kusonga mbele hatua inayofuata.

Chanzo: www.habarileo.co.tz