Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba kazi moja tu kwa Merrikh

034b91f8a1b55b263f1cf7e2b8cf6c7e Simba kazi moja tu kwa Merrikh

Sat, 6 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika Simba leo wako ugenini Khartoum Sudan kucheza na Al Merrikh ya huko katika mchezo wa tatu wa makundi.

Simba kinara wa kundi A kwa pointi sita itashuka dimbani ikiwa na morali ya juu baada ya kufanya vizuri katika michezo kadhaa iliyopita ya Ligi Kuu na hiyo ya kimataifa.

Michezo mitano iliyopita kwenye ligi kwa wekundu hao imeshinda minne na kupata sare moja. Wanashika nafasi ya pili kwa pointi 45 katika michezo 19 nyuma ya vinara Yanga wanaoongoza kwa pointi 49 katika michezo 22.

Katika kundi A, Simba ndiye mbabe akishinda michezo miwili dhidi ya AS Vita bao 1-0 ugenini na dhidi ya Al Ahly bao 1-0 nyumbani kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa.

Mchezo huo wa leo unaweza kuwa mgumu hasa kwa wenyeji watakaokuwa na presha ya kutafuta matokeo mazuri baada ya kutoka kupoteza michezo miwili dhidi ya Al Ahly ugenini walifungwa mabao 3-0 na dhidi ya Vita mabao 4-1 nyumbani kwao.

Merrikh wanahitaji matokeo mazuri lakini wanakutana na Simba ambao pia wanataka kuendeleza ubabe kwa kushinda au kupata sare wakiwa na lengo lao la kufanya vizuri na kwenda hatua za juu.

Simba chini ya Kocha Didier Gomes imekuwa ikionesha nidhamu kwa wapinzani kwa kulinda lango lao na kushambulia kwa kushtukiza mbinu iliyowasaidia katika michezo hiyo miwili ya kimataifa.

Hawatakuwa na presha wakijua wazi tayari wana pointi sita kwa hiyo wakipata ushindi au sare kwao ni faida kubwa ingawa hata wakipoteza bado watakuwa hawako vibaya.

Wapinzani hao wa Simba sio wabaya wanafanya vizuri kwenye Ligi Kuu ya Sudan wakishika nafasi ya pili kwa pointi 25 katika michezo 11 nyuma ya kinara Al Hilal yenye pointi 28.

Ni timu nzuri yenye uzoefu sawa na Simba katika michuano hiyo iliwahi kufika hatua tofauti za juu miaka ya nyuma ila sasa inakutana na wenzao ambao pia, ni bora na wana jambo lao. Mchezo utakuwa wenye ushindani mkubwa ila yeyote ana nafasi ya kushinda.

Chanzo: www.habarileo.co.tz