Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba kama sio mabingwa

0a7e2cae302af4a9bd393ee0ee7ed82f.png Simba kama sio mabingwa

Fri, 24 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

UNAWEZA usiamini kama Simba ndiyo Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, kutokana na matokeo yasiyoridhisha wanayoendelea kukutana nayo kuelekea ukingoni mwa ligi hiyo, baada ya jana kutoa suluhu ya nne dhidi ya Coastal Union pamoja na kupoteza mchezo mmoja katika michezo sita ya mwisho.

Simba ilitoa suluhu tatu mfululizo dhidi ya Tanzania Prison, Ndanda na Namungo, kabla ya kufungwa na Mbao mabao 3-2 na kushinda dhidi ya Alliance mabao 5-1, na kupata suluhu nyingine jana.

Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani Tanga, alishuhudiwa nyota Meddie Kagere akikabidhiwa tuzo yake ya mchezaji bora wa mwezi Machi kabla ya kuanza kwa mchezo huo.

Dakika ya 75, beki Pascal Wawa alioneshwa kadi nyekundu kwa kitendo cha utovu wa nidhamu kufuatiwa kudundisha mpira kwa hasira baada ya kumchezea Ayoub Lyanga madhambi kisha kutokubaliana na maamuzi ya mwamuzi wa mchezo huo na kumpa kadi hiyo.

Simba ilijaribu kwa hali zote kutaka kuondokana na jinamizi la sare kwa kutengeneza mashambulizi kutoka kila kona ya uwanja, hata hivyo wapinzani wao ambao pia hawakuwa na matokeo mazuri kwenye michezo yao iliyopita walikuwa imara zaidi. Dakika ya 80 mshambuliaji Kagere nusura aandike bao la kuongoza kufuatia shuti lake alilopiga akiwa kwenye eneo la hatari kugonga mwamba na mpira kutoka nje.

Sio hivyo tu Coastal Union hawakuwa nyuma kutafuta matokeo, walitumia mipira mirefu wakati wote, huku winga Ayoub Lyanga akionekana kuwa mwiba zaidi kwa mabeki wa Simba. Simba sasa itamaliza mchezo wa mwisho dhidi ya Polisi Tanzani mchezo utakaopigwa mjini Moshi, na baada ya hapo itasubiri mchezo wao wa fainali ya Kombe la FA.

Katika mechi zingine jana; Lipuli iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting wakati Polisi Tanzania ilifungana 1-1 na JKT Tanzania, huku Alliance ikitoka sare ya 2-2 na Ndanda.

Chanzo: habarileo.co.tz