Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba inakosea hapa kimataifa

46050 Pic+simba Simba inakosea hapa kimataifa

Mon, 11 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa JS Saoura ya Algeria ni ishara tosha ya kazi ngumu ambayo benchi la ufundi la Simba itapaswa kurekebisha katika safu yake ya ulinzi.

Kwa mara nyingine makosa ya namna ileile yamekuwa yakifanywa na Simba katika idadi kubwa ya mechi zake msimu huu na juzi usiku yalijirudia na kujikuta ikipoteza mchezo huo muhimu wa ugenini.

Endapo Simba ingepata ushindi ungeiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kukosa mbinu za kuhimili washambuliaji wenye kasi, kukosa utulivu na kujisahau kwa kutotimiza majukumu ya kukaba mpira unapokuwa langoni mwao ni miongoni mwa makosa yaliyojitokeza katika mchezo huo.

Simba imekuwa ikipata wakati mgumu mbele ya timu inayoshambulia kwa kasi kwani wachezaji wake hasa wale wanaocheza idara ya ulinzi hawana mbinu za kuwadhibiti na kujikuta wakilazimika kucheza rafu zinazochangia kuonyeshwa kadi na kusababisha adhabu ndogo au kubwa ya pigo la penalti.

Katika mchezo wa juzi, JS Saoura Ilipata bao moja lilitokana na penalti iliyosababishwa na rafu iliyochezwa na Mohammed Hussein 'Tshabalala’ dakika ya 50 katika eneo la hatari la Simba.

Pia kiungo Jonas Mkude na Paul Bukaba walionyeshwa kadi za njano kwa makosa ya kucheza rafu.

Tatizo jingine lililojionyesha katika  mchezo huo ni kutokuwa na utulivu katika safu ya ulinzi ambapo kila iliposhambuliwa mabeki waliokoa vibaya mipira na kunaswa kirahisi na JS Saoura ambayo iliweka kambi ya mashambulizi langoni mwa Simba.

Bao la kwanza la JS Saoura lilitokana na uzembe wa wachezaji wa Simba kutomkaba Sid Cherif ambaye alinasa mpira uliookolewa na Bukaba na kupiga shuti lililojaa wavuni.

 

Wasikie Kipingu, Mayay

Matokeo hayo yalimuibua aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Idd Kipingu ambaye alitaja sababu kubwa mbili zilizoigharimu Simba.

Kipingu alisema eneo la kiungo lilipoteza pasi nyingi na mabeki walikosa nidhamu ya ukabaji.

Mchambuzi Ally Mayay alisema Simba ilikosa nidhamu ya ulinzi ambayo ilikaribisha mashambulizi mengi langoni mwao ingawa alisifu mbinu za kocha Patrick Aussems.

Mayay alisema Simba ina nafasi ya kushinda mechi ya mwisho na AS Vita ya DR Congo endapo itacheza soka ya kumiliki mpira.

Mchambuzi Alex Kashasha ‘Mwalimu Kashasha’ alisema kuwa AS Vita inacheza soka ya kufunguka, hivyo Simba inatakiwa kucheza kwa umakini dakika zote 90.



Chanzo: mwananchi.co.tz