Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba hii na Yanga hii sio zile

20003 Pic+simba TanzaniaWeb

Mon, 1 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Tambo, kebehi na kejeli za miezi, wiki, siku na sasa saa, majibu yake yatapatikana leo baada ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Taifa wakati timu hasimu za Simba na Yanga zitakapoonyesha kazi.

Mabingwa hao watetezi ambao ndio wenyeji wa mchezo huo utakaoanza saa 11:00 jioni pamoja na Yanga, kila upande unakuja kivingine wakiwa na wachezaji wapya, makocha wapya ambao wanasubiriwa kwa hamu mashabiki kuona nani atamwonea mwenzake.

Yanga hii ina maingizo mapya ya akina Herietier Makambo, Feisal Salum’Fei Toto’, Nkizi Kindoki wakati Simba ina ingizo la Meddy Kagere, Cletus Chama, Marcel Kaheza na Adam Salamba wanaopewa nafasi kubwa ya kucheza. Timu zote zina maingizo mengine mengi.

Mbali na maingizo mapya, pia kuna wachezaji wengine ambao wamerejea katika vikosi hivyo kama Mrisho Ngassa aliyeko Yanga na Deogratius Munishi’Dida’ anayeichezea Simba ambao kwa nyakati tofauti waliondoka kwenye timu hizo.

Uimara na udhaifu wa vikosi

Yanga inaingia katika mchezo huo huku ikijivunia safu kali ya ushambuliaji iliyo na Makambo aliyefunga mabao mawili kwenye ligi na Ibrahim Ajib aliyefunga moja na kutoa pasi nne za mabao.

Wachezaji hawa wameonekana kucheza kwa maelewano makubwa katika michezo ya hivi karibuni na kama wataendelea hivyo katika mchezo wa leo basi Simba inabidi wajipange.

Pia safu ya kiungo ya Yanga ina Mzanzibar Feisal Salum ‘Fei Toto’ nayo imeimarika hivyo inaweza kuwadhibiti Simba leo ambao katika michezo mingi baina yao huwa inatawala eneo hilo.

Hata hivyo Yanga inaweza ikapata shida upande wa beki ya kulia anakocheza Paul Godfrey ambaye hana uzoefu na mechi kubwa kama hiyo baada ya Juma Abdul kuwa majeruhi na kuukosa mchezo wa leo.

Kwa upande wa Simba kukosekana kwa nahodha John Bocco itakuwa pengo kwa wekundu wa Msimbazi na kumtegemea zaidi Emmanuel Okwi na Meddy Kagere.

Bocco ana mabao mawili kwenye ligi wakati Kagere akiwa na manne huku Okwi akiwa hajafunga bao lolote na mara kadhaa huibukia kwenye mechi ya watani.

Safu ya kiungo ya Simba inayoongozwa na Jonas Mkude na ikinogeshwa na Chama itaendelea kuwa imara huku safu ya ulinzi nayo ikiwa ngangali.

Hata hivyo tatizo kubwa la Simba linaweza kuwa kwa beki wake Serge Pascal Wawa ambaye licha ya kuwa ni mzoefu na anatumia akili lakini kasi yake ndogo ya kukimbizana na washambuliaji kama Ngassa inaweza ikaigharimu timu hiyo.

Itakaowakosa

Simba itawakosa Bocco mwenye kadi nyekundu,Muzamiru Yassin na Hassan Dilunga walio majeruhi wakati Yanga itawakosa Juma Abdul na Juma Mahadhi ambao nao ni majeruhi.

Makocha

Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema watacheza soka la pasi za haraka ili kumiliki mpira muda mwingi wa mchezo.

“Kama tukimiliki mpira muda mwingi itafanya tusishambuliwe sana na wapinzani wetu.

“Tumejiandaa vizuri kushinda mchezo huo kwani wachezaji wangu wameonekana kuelewa kile ninachowafundisha mazoezini.Mashabiki waje kwa wingi kutusapoti ili kuwapa hamasa wachezaji’alisema Aussems.

Kocha wa Yanga,Mwinyi Zahera alisema”Hakuna ninachokihofia kwa wapinzani wetu kwani ni timu ya kawaida kama zilivyo nyingine.Kikosi changu kiko imara na tuko tayari kwa mchezo”alisema Zahera.

Wadau

Kocha wa zamani wa Kagera Sugar na Njombe Mji, Mrage Kabange alisema: ”Ukiingalia Yanga katika mechi za karibuni wamebadilika, Ajib ataendelea kuibeba Yanga, Tambwe pia amerudi, kuna Makambo hivyo inaonyesha jinsi gani Yanga ina watu wa kazi.

“Pia Simba nao wako vizuri kuna Emmanuel Okwi na Meddy Kagere ingawa itapata pigo kwa kumkosa Bocco lakini uzuri wa Simba ina kikosi kipana,” alisema Mrage.

Naye winga wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema mchezo huo ni maalum kwa wachezaji kujijengea heshima.

“Ujue mchezo wa Simba na Yanga unaweza kukung’arisha au kukuporomosha hivyo ni wajibu wa kila mchezaji wa timu hizo kucheza huku wakitambua hilo.

“Wacheze kwa kiwango bora ili kujenga heshima kama ilivyokuwa kwa Abdallah Kibadeni na Sunday Manara ambao hadi leo wanaendelea kukumbukwa,” alisema Chambua.

Chanzo: mwananchi.co.tz