Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba hii, acha tu!

33165 Pic+simba Tanzania Web Photo

Mon, 24 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wamekaa. Ilikuwa hakuna jinsi wala namna nyingine zaidi ya Simba kuilaza Nkana Red Devils katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba waliokuwa wamefungwa mabao 2-1 mchezo wa kwanza uliofanyika mjini Kitwe, Zambia siku 10 zilizopita, waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 na kuwatupa nje Nkana kwa jumla ya mabao 4-3.

Kwa hatua hiyo, Simba moja kwa moja inaingia hatua ya makundi na sasa itasubiri droo ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) itakayopangwa Desemba 28 mjini Cairo, Misri.

Miamba mingine iliyoingia 16 Bora na Simba ni pamoja na TP Mazembe ya DR Congo, Al Ahly na Ismailia (Misri), Wydad Casablanca (Morocco), Esperance (Tunisia), Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates (Afrika Kusini), CS Constatine (Algeria), Lobi Styars (Nigeria) na FC Platinum ya Zimbabwe.

Matokeo ya jana yanaifanya Simba kuendeleza ubabe kwa Nkana ambayo haijawahi kuifunga kwenye ardhi ya Tanzania kadhalika Simba haijawahi kuifunga Nkana ikiwa kwake Zambia.

Mashabiki hawakuamini kilichotokea

Mashabiki wa Simba walipigwa na butwaa na kushindwa kutoka uwanjani baada ya dakika 90 kwa kutoamini kilichotokea baada ya bao la kisigino la Cletous Chama dakika ya 88.

Chama alifunga bao hilo lililoihakikishia Simba nafasi ya kusonga mbele hatua ya makundi baada ya kupata pande la mtokea benchi, Hassan Dilunga aliyekuwa akihaha kuhakikisha anaibeba Simba.

Mashabiki walianza kuamini mchezo utamalizika kwa Simba kushinda 2-1 na kinachofuata ni matuta ndipo Chama akafuta mawazo hayo.

Mchezo wenyewe

Nkana iliwashtua Simba kwa kufunga bao la kuongoza dakika ya 16 lililowekwa kimiani na Walter Bwalya aliyeunganisha krosi ya Harrison Chisala aliyetokea upande wa kushoto kwa kumpiga chenga Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Bao hilo liliwazindua Simba na kusaka bao kwa nguvu na juhudi zao zilizaa matunda dakika 28 baada ya Jonas Mkude kusawazisha kwa shuti kali la mita 30 lililokwenda moja kwa moja wavuni huku kipa Chibwe akishangaa limempitaje.

Simba iliendelea kushambulia na dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza, Meddie Kagere aliifungia Simba bao la pili kwa kichwa akimalizia krosi ya Nicholas Gyan iliyotokana na mpira wa kona fupi iliyochongwa na Chama.

Kipindi cha pili kilianza kwa Nkana kujaribu kujilinda zaidi na kushambulia kwa kushitukiza jambo lililowapa mwanya kwa Simba kushambulia zaidi. Kila upande ulifanya mabadiliko kadhaa na kushambuliana mfululizo kabla ya Simba kupata bao hilo lililowanyong’onyeza kabisa Nkana walioingia nchini tangu Jumanne iliyopita.

Mashabiki Yanga watulizwa

Licha ya Simba kuwakilisha Tanzania, mashabiki wachache wa Yanga waliojitokeza uwanjani walijikuta wakitoka kwa aibu baada ya kipindi cha kwanza kuonekana kuwashangilia kwa nguvu Nkana, huku wakiliimba jina la beki wao wa zamani, Hassan Kessy.

Mtu pekee aliyewanyamazisha mashabiki hao ni Chama aliyefunga bao la tatu lililoivusha Simba hadi makundi wakiweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza makundi mara mbili, kwani awali walilingana na Yanga iliyokuwa ya kwanza kucheza hatua hiyo mwaka 1998.

Bao la Chama lilipokewa kwa shangwe na makocha wa Simba na hasa Aussems aliyeonekana akirukaruka kwa furaha huku akikumbatiana na wachezaji wake.

Aussems ana kila sababu ya kushangilia kwani moja ya masharti ya mkataba wake ni kuifikisha mbali Simba ili aongezewe mkataba mpya baada ya huu wa mwaka mmoja unaomalizika mwishoni mwa msimu huu.

Kessy aipa neno Simba

Beki wa Nkana, Hassan Kessy ambaye alipata kuiitumikia Simba kabla ya kujiunga na Yanga, aliwapongeza Simba kwa ushindi lakini akaonya kwamba wanapaswa kujipanga na kuongeza umakini katika hatua ya makundi kwani ni kugumu.



Chanzo: mwananchi.co.tz