Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba heshima, Morrison ang’aa Kagera

SIMBA Simba heshima, Morrison ang’aa Kagera

Thu, 9 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yakataa sherehe za ubingwa wao kuwekwa doa kama ilivyokuwa msimu uliopita...

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu wa 2019/20, Simba ya jijini Dar es Salaam, wameendelea kuupa heshima ubingwa wao baada ya kutoka suluhu na Namungo FC katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Majaliwa ulioko Ruangwa mkoani Lindi jana.

Sare hiyo imeifanya Simba ambayo iliwapumzisha nyota wake mbalimbali wa kikosi cha kwanza ifikishe pointi 81 huku Namungo yenyewe iweke kibindoni pointi 60 na kuendelea na kampeni ya kumaliza kwenye nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Simba wamekabidhiwa kombe la ubingwa wa msimu 2019/20 pamoja na medali na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Khamisi Kigwangwala ambaye aliongozana na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania ( TFF), Wallace Karia na wadhamini wakuu, Vodacom.

Abeid Athumani wa Namungo aliteuliwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo ya jana na kupata zawadi ya Sh.500, 000 kutoka katika benki ya KCB, ambao ni mmoja wa wadhamini wa ligi hiyo.

Licha ya Simba kupata sare ya tatu mfululizo, inamaliza msimu huu ikivuna pointi nne kutoka kwa Namungo baada ya kupata ushindi wa mabao 3-2, katika mchezo wa kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam.

Wenyeji Namungo walianza kwa kasi mchezo huo lakini golikipa wa Simba, Beno Kakolanya aliwahi kupangua shuti kali iliyopigwa na mshambuliaji, Steve Nzigamagabo dakika ya pili na kuwanyima bao la mapema.

Namungo waliendelea kulishambulia lango la Simba kupitia kwa Hashim Manyanya lakini Kakolanya kwa mara nyingine alipangua shambulizi hilo na Meddie Kagere akauondoa mpira jirani na goli lao dakika ya tisa.

Simba ilijibu shambulio hilo kupitia kwa Kagere lakini golikipa wa Namungo, Nurdin Balora, aliwahi kupangua shuti la Mnyarwanda huyo aliyekuwa katika nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 10 huku dakika ya 17 Kagere akapiga pembeni baada ya kuuwahi mpira kutoka kwa Khamisi Khalifa wa Namungo.

Dakika ya 18 Mbrazil, Tairon Santos aliwahi kutoa nje mpira uliopigwa na Abeid Athumani wa Namungo na kuwanyima tena wenyeji nafasi ya kufunga huku Simba ikipoteza nafasi ya kufunga baada ya mpira wa kichwa uliopigwa na Yusuph Mlipili kutoka nje dakika ya 26.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ile ile lakini Lucas Kikoti aliinyima timu yake bao baada ya mpira wa kwanza wa faulo uliopigwa dakika ya 53 kuishia mikononi kwa Kakolanya huku faulo ya pili dakika moja baadaye ikipaa langoni na kutoka nje.

Dakika ya 61 Kikoti tena alipiga nje akiwa jirani na Kakolanya wakati mabeki wa Simba wameshapotea na kupoteza nafasi ya kupata bao la kuongoza huku Balora akidaka krosi ya Ajibu, lakini Namungo wataiwaza nafasi aliyoipoteza Kikoti baada ya Kakoanya kuokoa mpira wakiwa wamebaki wawili dakika ya 64.

Kagere akiunganisha pasi fupi ya Deo Kanda, alikosa bao baada ya Balora kudaka shuti hilo dakika ya 88 huku sekunde chache shuti la Athumani wa Namungo likigonga mwamba na kurudi uwanjani.

Namungo; Nurdina Balora, Minza Christoms, Edward Charles, Steven Dua, Carlos Protas, Hamisi Khalifa, Hashim Manyanya/ Jamal Issa (dk 72),Steve Nzigamagabo, Bigirimana Blaise/ Jovin Kelvin (dk 29), Lucas Kikoti na Abedi Athumani.

Simba; Beno Kakolanya, Haruna Shamte/ Hassan Dilunga ( dk 64), Mohammed Hussein/Shiza Kichuya (dk 73), Tairon Santos/ Gadiel Michael ( dk 51), Said Ndemla, Miraji Athumani ' 'Sheva', Muzamiru Yassin, Meddie Kagere, Ibrahim Ajib/ Cyprian Kipenye ( dk 72), na Francis Kahata/ Deo Kanda ( dk 64).

Wakati huo huo, Yanga jana iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezea mjini Bukoba.

Kosa lililofanywa na beki wa Kagera Sugar, Erick Kyaruzi la kuukosa mpira na kupiga hewa, ukamkuta Benard Morrison akiwa kwenye wingi ya kulia, alimchambua kipa Benedict Tinoco na mpira kujaa wavuni kwenye dakika ya 78.

Ilikuwa ni sekunde chache tu baada ya Morrison huyo huyo kupiga shuti kali lililoonekana kwenda wavuni, lakini kipa Tinoco alipangua.

Nafasi ambazo Kagera Sugar watajutia zaidi ni dakika ya 35, Kelvin Sabato alipopiga shuti lililookolewa kwa ustadi na kipa Farouk Shikalo, huku dakika ya 62, Shikalo akiokoa kwa mguu krosi iliyounganishwa na Abdallah Seseme.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live