Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba chupuchupu

6866 SimbaLipuli TZW

Sun, 22 Apr 2018 Chanzo: habarileo.co.tz

VINARA wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara, Simba jana walipunguzwa kasi baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Lipuli katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Samora, Iringa.

Lipuli ilikuwa ya kwanza kupata bao la lililofungwa na Adam Salamba dakika ya 32 na Simba wakisawazisha dakika ya 66 likifungwa na Laudit Mavugo.

Simba itaendelea kuwa kileleni mwa msimamo ikifikisha pointi 59 katika michezo 25 iliyocheza huku mahasimu wao Yanga wanaotarajiwa kucheza leo wakiendelea kuwa katika nafasi ya pili kwa pointi 47 katika michezo 22 waliyocheza.

Hii ni mara ya pili wekundu hao wanalazimishwa sare ya bao 1-1 na timu hiyo baada ya raundi ya kwanza kupata matokeo ya aina hiyo kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Kipindi cha kwanza timu zote zilicheza vizuri na kushambuliana kwa zamu ambapo Lipuli walipata bao la uongozi lililodumu hadi kumalizika kwa kipindi hicho.

Kipindi cha pili Simba ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Juuko Murshid na kuingia Mavugo aliyeisawazishia Simba bao baada ya kupata mpira wa kona uliopigwa na Shomari Kapombe.

Timu zote zilicheza kwa kushambuliana kwa zamu na kutengeneza nafasi kadhaa ambazo kila mmoja alikuwa na nafasi ya kupata magoli zaidi lakini walizipoteza. Baada ya Lipuli kupata bao la uongozi walitengeneza nafasi nyingine dakika ya 35 na 36 kwa Salamba lakini hawakuwa makini.

Kwa upande wa Simba dakika ya 29 na 38 Shiza Kichuya alipata nafasi na kushindwa kuzitumia ipasavyo na dakika ya 79 Mavugo alipaisha mpira. Lakini hadi dakika 90 zinamalizika matokeo yaliendelea kubaki 1-1 kila timu ikicheza kwa kiwango kizuri.

Simba: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Juuko Murshid/Mavugo dk.45, Yusufu Mlipili, Shomari Kapombe, Shiza Kichuya, James Kotei, Asante Kwasi, Nicholaus Gyan, Emmanuel Okwi na Jonh Bocco.

Lipuli: Mahamed Yusuph,Steve Mganga, Paul Ngalema, Ally Mtoni, George Owino, Fred Tangalo, Daluwesh Saliboko, Mussa Nampaka, Adam Salamba, Malimi Busungu na Seif Karie.

Chanzo: habarileo.co.tz