Tanzania, ikiwa nchi ya mfumo wa vyama vingi siasa vya siasa imekumbana na mambo mengi katika ushindani wa kisiasa, yapo mazuri na mengine ya kukatisha tamaa.
Katika uwanja wa ushindani wa vyama hivyo, kumekuwapo na maeneo ambapo wanasiasa wa vyama hushirikiana kwa upendo lakini katika baadhi hukamiana kama vile ni uhasama.
Mathalan, katika Bunge unaona wabunge wakijenga hoja za kubezana na kafedheheshana na mara chache utaona wanasiasa hao – wa chama tawala na upinzani wakiungana na kuwa kitu kimoja kwa maslahi ya Taifa, badala ya vyama vyao.
Lakini wakati hali ikiwa hivyo, kwenye masuala ya michezo mambo yanakuwa tofauti, hasa katika mechi ya za watani wa jadi, Simba na Yanga.
Jumamosi iliyopita wanasiasa wa vyama tofauti, CCM na Chadema ambao ni mahasimu wakubwa majukwaani walikutanishwa na mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar
es Salaam.
Mchezo huo licha ya kulimalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0, bado hiyo haikuondoa furaha yao waliochukuliwa kwa utani wao wa siku zote wa jadi.
Baadhi ya wanasiasa walioshuhudia mtanande huo ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha wote kutoka CCM.
Pia kutoka CCM walikuwapo wabunge, Mbunge wa Sengerema Willim Ngeleja, Mussa Hassan Zungu (Ilala), Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Kwa upande wa Chadema waliionekana ni Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Meya ya Ubungo, Boniface Jacob na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.
Hata mazungumzo ya wanasiasa hao hayakujikita kwenye masuala ya siasa yanayowagawa, bali katika utani wa mchezo huo.
Nyongo alilieleza Mwananchi kuwa yeye ni mpenzi wa michezo na hasa Simba, hivyo alikata kiu yake kwa kupata ushindi.
“Timu zote zilicheza vizuri na sikutegemea kama Yanga leo (juzi) wangecheza vizuri namna hii, ila tuwape sifa kwa jinsi wanavyocheza. Kwa kweli ilikuwa wafungwe magoli mengi lakini wamepunguza idadi ya magoli.
“Mimi na wabunge wenzangu ambao ni mashabiki wa Simba tuna kundi letu, tunaisapoti Simba kwa namna tunayoweza. Vilevile mimi ni mwenyekiti wa Chama cha Mpira mkoa wa Simiyu, ninapenda mpira na ninausapoti sana.
Mchungaji Msigwa ambaye pia ni shabiki wa Simba, alisema mchezo ulikuwa mzuri zaidi kwenye ushabiki kuliko uwanjani, licha ya kwamba Simba ilicheza vizuri kuliko Yanga na ilistahili kushinda.
“Nimefurahia ushindani wa kiushabiki nje ya uwanja, kwani ilikuwa burudani nzuri zaidi kuliko ndani ya uwanja,” alisema Msigwa.
Meya Jacob alisema mchezo ulikuwa mzuri na tafsiri mashabiki wa Yanga kwenda wachache uwanjani ni kwamba wanaujua moto wa Simba.
Nje ya uwanja, pia wanasiasa walishiriki furaha ya mchezo tofauti na ujumbe wa kisiasa waliozoea kutoa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi aliandika kwenye mtandao wake wa Instagram baada ya mchezo: “Ni kweli mmeshinda lakini ubingwa mtausikia redioni.”
Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule “Professor Jay” aliandika katika Instagram kuwa: “Leo tumewabeep tu maana nyinyi sio levo (level) yetu. Sasa tunawasubiri wale Wacongo wenu waliowatuma muimbe sana Bolingo.”
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alindika pia Instagram: “Naona ‘Friends Of Simba’ ule mpango wenu wa nje ya Uwanja umefanikiwa. Kwa kweli sishangai nje ya Tanzania mkipigwa khamsa (tano) maana huko huwa hamjui pa kupita.”
Lakini mwenyeji wao, Makonda kupitia Instagram aliandika: “Nimepokea taarifa kutoka kwa Mrisho Gambo, Ridhiwani Kikwete (Mbunge Chalinze), Jerry Muro (DC-Arumeru), Ally Hapi ya kwamba wako Yanga kwa heshima ya wazazi wao, ila kama ni mapenzi yao basi Yanga si timu tena.