Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga zamlilia Magufuli

21f74d99190b5b06ce4746e3f368de18.jpeg Simba, Yanga zamlilia Magufuli

Fri, 19 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TIMU zote za Ligi Kuu Tanzania zikiongozwa na vigogo wa soka nchini Simba, Yanga na Azam FC zimeonesha kuhuzunishwa na kifo cha Rais John Magufuli na kutuma salamu za rambirambi kuungana na watanzania wengine.

Rais John Magufuli alifariki dunia juzi usiku na msiba wake kutangazwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan. Kupitia mitandao ya kijamii ya klabu hizo, kila mmoja ameeleza kuhuzunishwa kwake na msiba huo mzito.

“Uongozi wa klabu ya Simba umepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Rais wetu Dk John Magufuli tunawaomba watu wote tuendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi,”ilisema Simba.

Simba iliweka nukuu ya kiongozi huyo alipokwenda kuwakabidhi taji la Ligi Kuu waliloshinda msimu wa mwaka 2017/2018 aliyosema “kama kiongozi wenu nitafurahi sana siku moja siku mkiniita hapa kuja kukabidhi kombe la Afrika lililochukuliwa na timu yoyote katika nchi yetu,” “Niwaombe Simba mkawe wa kwanza kuleta Kombe la Afrika hapa Tanzania.”- Hayati Rais Magufuli.

Msemaji wa klabu hiyo Haji Manara jana aliweka ujumbe huu na kuandia: “Umeondoka huku tukiwa hatujatimiza maagizo yako, lakini kifo chako kimekuja ktk kipindi ambacho nafasi ya kutekeleza hayo maelekezo ni kubwa na uwezo huo tunao,”

“Mh Rais wetu uliyedondoka kama ute wa Mshumaa,tunakuahidi wanasimba kwamba, tutacheza mashindano haya ya ubingwa wa Afrika kwa nguvu kubwa na kwa ari ya hali ya juu ili kukuenzi kwa hii changamoto uliyotuachia,”.

“Hii kwetu iongoze umoja wetu kama klabu na maneno haya tuyaishi kama wanamichezo, kama wanasoka na kama wanasimba ili hatimae tufanikiwe kubeba taji la ubingwa wa Afrika,” Kocha wa Simba Didier Gomes naye alituma salamu za rambirambi kwa watu wa Tanzania akisema fikra na dua zake zipo kwa Rais John Magufuli.”

Kwa upande wa Yanga, uongozi wake ulisema umepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo hicho. “Kwa niaba ya wanachama, mashabiki na wapenzi wa Yanga tunatoa pole kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu, Familia, Ndugu, Jamaa na marafiki na watanzania wote,” waliweka ujumbe huo kwenye mtandao wao wa Instagram.

Kwa upande wa Azam FC, nao walisema wamepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo hicho wakisema wanatoa pole kwa wafanyakazi wao wote, mashabiki na wapenzi kwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu na Serikali kiujumla, watanzania, ndugu, jamaa na marafiki, kwa kumpoteza kiongozi huyo shupavu wa Taifa.

“Azam FC tunaungana na watanzania wote kuomboleza kifo cha mpendwa wetu, kwa kutambua na kuheshimu mambo makubwa aliyolifanyia Taifa hili kwa muda wote aliohudumu ndani ya Serikali,”alisema.

Wengine waliotoa salamu zinazofanana na hizo ni Biashara United, Polisi Tanzania, Kagera Sugar, Ihefu, Mbeya City, Ruvu Shooting, Namungo, Tanzania Prisons, Biashara United na Mtibwa Sugar

Chanzo: www.habarileo.co.tz