Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga zabanwa

90826 Simbayanga+pic Simba, Yanga zabanwa

Mon, 6 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mchuano mkali waendelea katika vita ya kujinasua na janga la kushuka daraja...

VIGOGO wa soka nchini, Simba na Yanga zilishindwa kufurukuta ugenini baada kulazimishwa suluhu na timu za Ndanda FC ya Mtwara na Biashara United ya Mara, katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara zilizochezwa jana.

Mabingwa wa msimu huu, Simba, wakiwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona waliondoka na pointi hiyo moja huku wenyeji Ndanda walioko katika hatari ya kushuka daraja wakionyesha kandanda safi.

Kwenye mechi hiyo, Simba ilionekana kucheza mchezo wa taratibu na pasi nyingi, huku Ndanda ikionekana inatafuta ushindi au japo sare ili kujiongozea hazina ya pointi kwa ajili ya kujiondoa kwenye janga la kushuka daraja.

Ilikuwa ni sare ya pili mfululizo kwa Wekundu wa Msimbazi, baada ya Jumapili ya Juni 28, mwaka huu kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa CCM, Sokoine jijini, Mbeya.

Dakika ya 29, Luis Miquissone wa Simba alipiga shuti la kustukiza, lakini lilitemwa na kipa, Ally Mustapha 'Barthez', kabla ya kuokolewa na mabeki wa Ndanda huku nahodha wa mabingwa hao, John Bocco alikaribia kuipatia timu yake bao dakika ya 38, baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi iliyopigwa na Deo Kanda, lakini mpira ulitoka kidogo nje ya lango la Ndanda.

Simba ilikosa tena bao la wazi dakika moja kabla ya kwenda mapumziko, baada ya Kanda kupiga 'tik-tak', akiunganisha krosi ya Miquissone, lakini mpira ukatoka tena nje ya lango.

Miquissone ambaye kwenye mechi ya jana ndiye alikuwa kivutio kwa kucheza kandanda safi, nusura tena aifungie Simba bao dakika ya 71, alipopiga shuti lililowababatiza mabeki wa Ndanda na kurejea uwanjani.

Aishi Manula aliiokoa Simba kufungwa bao dakika ya 74 kutokana na shuti la juu lililokatika kama upinde wa mvua, lakini Manula aliruka juu kwa ustadi na kudokoa mpira ukatoka sentimeta chache juu ya lango la Simba na kuwa kona ambayo haikuwa na madhara.

Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 80 na kuendelea kukaa kileleni wakati Ndanda wamefikisha pointi 36 na kupanda hadi nafasi ya 17.

Kwenye Uwanja wa Karume, Musoma Yanga ilijiongezea pointi moja na kufikisha pointi 61, baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na wenyeji Biashara United ambayo ina rekodi nzuri ikiwa nyumbani msimu huu.

Timu zote zilicheza mchezo wa kukamiana, nguvu na mipira mirefu, kiasi cha kufanana kwa kila kitu.

Ditram Nchimbi alipiga mpira ovyo, dakika ya 47, akiwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga bao, baada ya mabeki wa Biashara United kujichanganya wakati dakika ya 55, wachezaji watatu wa Yanga, Lamine Moro, Nchimbi, na David Molinga, waliingia wenyewe nyavuni, wakiwa kwenye harakati za kutaka kuunganisha mpira wa faulo uliopigwa na Juma Abdul.

Dakika saba kabla ya pambano hilo limalizika, nusura Yanga iandike bao, baada ya Juma Makapu kupiga kichwa mpira wa kona uliopigwa na Patrick Sibomana, lakini ukapaa juu ya lango.

Yanga ilikuwa kwenye nafasi ya pili, kabla ya mechi ya jana usiku kati ya Azam FC dhidi ya Singida United, huku Biashara United ikiwa kwenye nafasi ya tisa kwa pointi 45.

Kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, Alliance FC ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar na matokeo hayo, yanawafanya wakazi wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro kufikisha pointi 38, wakati Alliance wao wana pointi 37, lakini timu zote zikitakiwa kupambana kujinasua na hatari ya kushuka daraja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live