Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Yanga  hakuna kulala

A26417f5d1dc2c09ca2f6080ffae5ab6.jpeg Simba, Yanga  hakuna kulala

Tue, 29 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WATANI wa jadi kwenye soka la Tanzania klabu za Simba na Yanga zimeingia kambini kujiandaa na mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao utapigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Jumamosi.

Simba ambao ndio vinara wa ligi hiyo wamedhamiria kushinda mchezo huo ili kutangazwa mabingwa kupitia mgongo wa watani wao Yanga na kulitetea taji hilo kwa msimu wa nne mfululizo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema maandalizi ya kujiandaa na mchezo huo yalianza jana jioni ikiwa ni siku moja baada ya timu hiyo kurejea Dar es Salaam ikitokea Ruvuma ambako walikwenda kucheza mechi ya nusu fainali ya FA dhidi ya Azam FC.

“Maandalizi ya mchezo unaofuata dhidi ya watani zetu Yanga tunaanza leo (jana) jioni, unajua tuliporudi kutoka Ruvuma tuliwapa mapumziko mafupi wachezaji na wote tutaingia kambini Bunju kujiandaa na mchezo huo ambao tumedhamiria kushinda,” alisema Rweyemamu.

Meneja huyo alisema ukimtoa kiungo Jonas Mkude, wachezaji wote wapo katika hali nzuri na hakuna majeruhi, hivyo ana amini kama hali itakuwa hivyo hadi siku ya mchezo itamsaidia kocha, Didier Gomes kuwa na uwanja mpana wa kuchagua wachezaji wa kuwatumia kwenye mchezo huo.

Alisema anajua kama hautakuwa mchezo mwepesi kwao na hata wapinzani wao Yanga, lakini dhamira yao kubwa ni kuhakikisha wanashinda ili kuweka kibindoni taji hilo ambalo litakuwa la nne mfululizo na la kwanza kwa msimu huu.

Wakati Simba wakiingia kambini Bunju, wapinzani wao Yanga nao walitarajiwa kuingia kambini jana jioni huko Avic Town, Kigamboni kujiandaa na pambano hilo, huku nao wakijitapa watapata ushindi kama walivyofanya kwenye mechi mbili zilizopita.

Meneja wa mabingwa hao wa kihistoria, Hafidh Salahe alisema wanatambua uzito wa mchezo huo na kwamba Kocha, Nasreddin Nabi, amemuhakikishia kwamba atazitumia vizuri siku zilizobaki ili kuhakikisha furaha ya mashabiki wao inaendelea hadi mwisho wa msimu kwa kupata ushindi.

“Hatuna majeruhi mpya zaidi ya Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Yassin Mustapha na Balama Mapinduzi, wengine watatu ambao tutawakosa ni nahodha Lamine Moro, Metacha Mnata na mshambuliaji Michael Sarpong hawa wakiwa na makosa ya utovu wa nidhamu,” alisema Hafidhi.

Alisema mchezo huo wameupa jina la vita sababu wamejiandaa kuhakikisha wanaondoka na pointi zote tatu ambazo ana amini zitasaidia kuwapunguza kasi wapinzani wao ambao wamebakiwa na mechi tano kumalizi ligi wakati wao Yanga wameipita Simba michezo miwili.

Awali, mpambano huo ulipangwa kupigwa Juni 8, Uwanja wa Mkapa lakini ilihairishwa baada ya kutokea mkanganyiko wa muda wa kuanza mchezo huo kufuatia taarifa ya kuusogeza mchezo huo kwa masaa mawili mbele kutoka saa 11 jioni na kutaka uchezwe saa 1:00 usiku, jambo ambalo Yanga waliligomea.

Chanzo: www.habarileo.co.tz