Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba SC hii hakuna kulala

8930 Simba+pic TZW

Tue, 12 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nakuru. Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba, wameweka wazi kuwa dhamira yao ni kucheza fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup, hivyo wanauchukulia kwa uzito mkubwa mchezo wa leo dhidi ya Kakamega Homeboys.

Simba ilitinga nusu fainali ya michuano hiyo, baada ya kuiondosha Kariobangi Sharks kwa mikwaju ya penalti 4-2 na leo itaivaa Kakamega Homeboys iliyoitoa Yanga kwa mabao 3-1.

Kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma alisema timu hiyo haikucheza vizuri mechi ya robo fainali lakini itakuwa na mabadiliko makubwa kwenye mchezo huo.

“Tulicheza vibaya kila mmoja wetu ameliona hilo. Hatuwezi kurejea tena kwa akili hiyo, wachezaji wote wameona tunahitaji kubadilika kwenye mechi ya mwisho,” alisema Djuma.

Kwa upande wake nahodha wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alisema hawatapenda kufika tena kwenye hatua ya penalti, hivyo watapambana kupata ushindi ndani ya dakika 90.

“Penalti siyo nzuri, ni kama bahati nasibu. Tulikuwa na mpango wa kushinda ndani ya dakika 90 tukashindwa dhidi ya Sharks lakini tutarejea kesho (leo) tukiwa tofauti ili tuweze kushinda,” alisema mchezaji huyo bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2016/17.

Singida United

Kwa upande wao Singida United wamekiri kuwa wanakutana na Gor Mahia ambayo ni timu kubwa, lakini wamekuja kupambana kuhakikisha wanakwenda hatua ya fainali.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hemedi Morocco alisema amebaini baadhi ya kasoro katika mechi ya kwanza, hivyo watabadilika ili kucheza vizuri dhidi ya Gor Mahia ambayo inapewa nafasi ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.

Hata hivyo, alisema kuwa bado hajawazoea vizuri wachezaji wake kwa sababu ndiyo kwanza anaanza kazi.

Naye nahodha wa timu hiyo, Nizar Khalfan alisema penalti ni kamari na hawatapenda mchezo wao dhidi ya Gor Mahia kufika hatua hiyo.

Wasikie Gor Mahia

Kocha msaidizi wa Gor Mahia, Zedekea Ottieno alisema mechi dhidi ya Singida United itakuwa ngumu kwa namna wanavyocheza ingawa haitakuwa kikwazo kwao kufika fainali.

“Utakuwa mchezo mgumu, nimewaona Singida United wanavyocheza. Tunajiandaa kama Gor Mahia na tuko tayari kutetea ubingwa wetu.

“Ukitaka kushinda lazima ufunge mabao. Tunataka kushinda mechi hiyo lazima tufunge mabao.

“Tunaendelea kupambana kuhakikisha tunapata ushindi mapema,” alisema Ottieno.

“Singida wana safu nzuri ya ulinzi ndiyo maana walicheza bila kufungwa. Kwenye mechi ijayo watakuwa wakijilinda zaidi dhidi ya safu yetu imara ya ushambuliaji, sidhani kama watamudu kasi yetu.

“Tutawaanzisha wachezaji wetu wa kikosi cha kwanza ambao walikosa mechi ya kwanza. Tunatarajia wataongeza nguvu kubwa kwenye timu ili tuweze kupata ushindi.

“Mshambuliaji wetu Jacque Tuyisenge amerejea na tuna amini anaweza kucheza mechi dhidi ya Singida. Atakuwa bora pia, ndio sababu tulimpa dakika chache kwenye mechi iliyopita,” alisema Ottieno.

Chanzo: mwananchi.co.tz