Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Mbao zapeta

38217 Simbapic Simba, Mbao zapeta

Fri, 25 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Gor Mahia kuvuliwa ubingwa wa mashindano ya Kombe la SportPesa na Simba kutoka uwanjani kufuzu nusu fainali, ni miongoni mwa matukio makubwa yaliyojiri kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Gor Mahia ya Kenya ambao walikuwa mabingwa watetezi wa mashindano hayo mara mbili mfululizo, walivuliwa taji hilo na Mbao FC ya Mwanza kwa kufungwa penalti 4-3.

Awali, timu hizo zilitoka uwanjani kwa sare ya bao 1-1 kabla ya kupigiana penalti ambazo kwa upande wa Mbao iliyofuzu nusu fainali, zilifungwa na Said Khamis, Raphael Siame, Hamimu Abdukarim na David Mwasa wakati Hashimu Ibrahim alikosa.

Penalti za Gor Mahia zilifungwa na Francis Kahata, Jacques Tuyisenge na Boniface Omond wakati Harun Shakavah na Shafik Batambuze walikosa.

Ukiondoa mchezo huo, Simba iliyocheza mechi hiyo kwa mara ya kwanza tangu iliporejea nchini ikitokea DR Congo ilipolala mabao 5-0 dhidi ya AS Vita, iliing’oa katika mashindano hayo AFC Leopards ya Kenya kwa kuwachapa mabao 2-1.

Simba inatarajiwa kumenyana na Bandari Kenya katika mchezo wa nusu fainali uliopangwa kuchezwa kesho.

Awali, kocha wa Bandari Ben Mwalala alisema alikuwa akitaka kucheza na Simba baada ya Yanga kutupwa nje katika mashindano hayo.

Kocha wa Simba Patrick Aussems, jana alianzisha sura mpya katika kikosi chake akiwatumia wachezaji wa kigeni waliokuja kufanya majaribio ya kusajiliwa.

Mshambuliaji Hunlede Kissimbo wa Togo na Lamine Moro wa Ghana walicheza mchezo huo ambao beki Moro alionekana kucheza vizuri kulinganisha na mwenzake ambaye alionekana kuwa mzito.

Kissimbo alishindwa kwenda na kasi ya mchezo na mara kwa mara alishindwa kucheza kwa uwiano mzuri na Emmanuel Okwi aliyekuwa mwiba kwa mabeki wa AFC Leopards.

Pia Aussems alimuanzisha kiungo nguli Haruna Niyonzima ambaye alicheza vizuri katika eneo la katikati akishirikiana na Jonas Mkude na Hassani Dilunga na Chama.

Kwa muda mrefu Niyonzima ambaye ni mchezaji mwandamizi wa Rwanda, amekuwa akisugua benchi baada ya kukosa namba katika kikosi cha kwanza. Lakini, jana alionyesha ukomavu kwa kucheza vyema na mara kwa mara alionekana akitoa pasi maridadi zilizofika kwa mchezaji husika.

Hata hivyo, Dilunga alianza kupigiwa kelele na mashabiki wa Simba dakika ya 65 baada ya kushindwa kufanya uamuzi wa haraka.

Mara kwa mara Dilunga akipoteza mipira kwa wapinzani ama kwa kupokwa au kutoa pasi fyongo ambazo zilinaswa na wachezaji wa AFC Leopards.

Kitendo cha mchezaji huyo kupoteza pasi, kilimlazimu Aussems kumtoa dakika ya 76 na nafasi yake kuchukuliwa na Mohammed Ibrahim.

Mchezo wenyewe

Simba ilipata bao dakika ya 13 lililofungwa na Okwi kwa shuti kali baada ya kuwalamba chenga mabeki wawili wa AFC Leopards kabla ya kutumbukiza mpira wavuni.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda, aliyekuwa akihaha uwanjani kusaka mabao, alifanya jitihada binafsi kwa kumpa pasi ya mwisho kwa Clatous Chama aliyefunga bao la pili dakika 47.

Simba ilishindwa kutumia vyema nafasi zilizotengenezwa na Okwi kupata idadi kubwa ya mabao, baada ya mipira mingi aliyopita kukosa mtu wa kuunganisha.

Kibao kiligeuka kwa Simba dakikam 45 za kipindi cha pili baada ya AFC Leopards kutulia na kutengeneza nafasi za mabao na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 61 ilipopata bao lililofungwa na Oburu Vincent.

Aussems alisema mchezo ulikuwa mgumu, lakini amepongeza juhudi za wachezaji wake ingawa alidai atakwenda kufanyia kazi kasoro zilizojitokeza katika safu ya ushambuliaji. AFC Leopards ililalamikia kitendo cha Simba kumtumia Moro katika mashindano hayo.



Chanzo: mwananchi.co.tz