Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Mazembe utamu uko hapa

50238 Pic+simba

Thu, 4 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya Simba kuvaana na TP Mazembe ya DR Congo katika mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, safu yake ya ushambuliaji inawapa matumaini ya kuwaduwaza mabingwa hao mara tano wa mashindano hayo.

Simba inayocheza na JKT Tanzania leo katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro, inatarajia kuikabili TP Mazembe ikiwa na safu kali ya ushambuliaji ambayo imeweka rekodi tofauti katika mashindano mbalimbali.

Rekodi ya kwanza ambayo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na ubora wa safu ya ushambuliaji ni ile ya Simba kupata ushindi katika mechi 10 mfululizo za Ligi Kuu msimu huu.

Katika mechi hizo 10 Simba imefunga mabao 25 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne, na matokeo haya yaliwapeleka kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 67, baada ya kucheza mechi 22.

Mbali na kuweka rekodi katika Ligi Kuu, pia imeweka rekodi nyingine kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kushinda mechi zote tatu walizocheza uwanja wa nyumbani na tangu hatua ya awali kwenye mashindano hayo Simba imefunga mabao 18 na kufungwa 17.

Katika Ligi Kuu anayeongoza kwa kufunga mabao katika kikosi cha Simba ni mshambuliaji Meddie Kagere mwenye mabao 14, akifuatiwa na nahodha John Bocco aliyefunga 11.

Pia Kagere anaongoza kwa kufunga mabao sita katika Ligi ya Mabingwa Afrika akifuatiwa na Clatous Chama (matano), Bocco (matatu), Emmanuel Okwi (mawili), Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Jonas Mkude kila mmoja amefunga bao moja.

TP Mazembe ambayo itakuwa wageni katika mechi ya Jumamosi, katika mechi 10 za mwisho kwenye ligi imefungwa mechi moja iliyopita dhidi ya St Eloi Lupopo ikilala kwa bao 1-0 na kushinda tisa.

Katika msimamo wa Ligi TP Mazembe ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 64, imecheza mechi 24, nyuma ya vinara AS Vita waliokuwa kileleni kwa pointi 65 wakicheza mechi 25.

TP Mazembe mbali na kupoteza mechi moja katika ligi imefunga mabao 27 na kufungwa sita. Mchezaji hatari wa kuchungwa ni Tresor Mputu ‘Mabi’ ambaye katika Ligi ya Mabingwa Afrika amefunga mabao manne.

Mputu baada ya kuzunguka katika timu mbalimbali Afrika na nje, mwaka 2016 alirejea TP Mazembe ambapo mpaka sasa amecheza mechi 27 na kufunga mabao 12.

Rekodi inaonyesha Mputu ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Ligi ya Mabingwa Afrika akifunga mabao 56.

Kauli ya Kocha Simba

Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema anajivunia wachezaji wake kuweka historia katika Ligi Kuu kushinda mechi 10 mfululizo bila.

Aussems alisema ameandaa kikosi imara cha kushinda mechi aliyodai itakuwa ngumu dhidi ya JKT Tanzania.

Alisema baada ya kumaliza mechi na JKT Tanzania atakuwa na fursa nzuri ya kuelekeza nguvu za kutosha katika mechi dhidi ya TP Mazembe.

“Tutaingia katika mechi hiyo bila ya kuwa na presha yoyote ila tutafanya maandalizi ya kiufundi zaidi kwa wachezaji wangu ili kucheza vizuri ili kuwa silaha yetu ya kupata ushindi katika mechi ya kwanza ambayo itatoa taswira ya mchezo wa marudiano,”alisema Aussems. Kocha huyo alisema ushindi wa mechi 10 za ligi umeongeza morali kwa wachezaji wake kujiandaa vyema kuikabili TP Mazembe aliyosema ni klabu kubwa Afrika.

“TP Mazembe ni timu kubwa kwa soka la hapa Afrika, wanafahamu umuhimu wa mashindano haya makubwa kwa ngazi ya klabu. Kwetu tunafahamu jambo hilo na tunafahamu mechi itakuwa ngumu kwa upande wetu,” alisema Aussems. Katika mchezo wake wa ligi uliopita, Simba ilipata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Mbao FC kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.



Chanzo: mwananchi.co.tz