Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba: Hatujui Nini Kiliwapata Yanga

SIMBA 1.png?fit=604%2C357&ssl=1 Simba: Hatujui Nini Kiliwapata Yanga

Tue, 11 May 2021 Chanzo: globalpublishers.co.tz

Simba: Hatujui Nini Kiliwapata Yanga May 11, 2021 by Global Publishers



UONGOZI wa Simba umesema kuwa haujui kilichowapata watani zao wa jadi Yanga kwa kushindwa kufuata mabadiliko ambayo walipewa muda mfupi kabla ya mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopaswa kuchezwa juzi.

Mei 8, ilipaswa uchezwe mchezo wa ligi kati ya Simba na Yanga ambapo muda wa awali ilikuwa ni saa 11:00 jioni, ulibadilishwa saa chache kabla ya mchezo huo baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa taarifa ya kupeleka mbele mpaka saa 1:00 usiku.

TFF ilieleza kuwa imetoa taarifa kwa timu zote mbili kuhusu mabadiliko ya muda huo kupitia kwa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).Yanga waligomea mabadiliko ya ghafla ya muda kwa kueleza kuwa kitendo hicho ni kinyume na kanuni ya 15 (10).



Kanuni hiyo inasema: “Muda wa kuanza mchezo (kickoff) utapangwa katika mazingira ya kawaida na kwa mazingatio maalum ya hali kwa michezo inayoonyeshwa kwenye televisheni, viwanja, na sababu nyingine yoyote muhimu.

Mabadiliko yoyote ya muda wa kuanza mchezo yatajulishwa ipasavyo kwa pande zote husika za mchezo angalau saa ishirini na nne kabla ya muda wa awali uliopangwa.

Michezo iliyo na mazingatio maalum, muda wa kuanza mchezo (kickoff) utazingatia mazingira husika.”Akizungumza na Championi Jumatatu, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alishangaa Yanga kugomea mchezo huo kwa kisingizio cha muda kusogezwa mbele.

Rweyemamu alisema: “Hatujui nini kiliwapata Yanga na kwa sasa siwezi kusema neno lolote kwa sababu wote tulipewa taarifa kuhusu mabadiliko ya muda kisha wenzetu wakaamua walichokifanya, hivyo sijui nini kiliwapata.

”Alipotafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli hakuweza kupokea simu, Ofisa Uhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz naye pia ilikuwa hivyohivyo.

Taarifa ya TFF iliyotolewa jana ilieleza kuwa TFF inaendelea kufanya vikao mbalimbali na vyombo vya Serikali kuhusu tukio hilo, pia itakutana haraka na klabu za Simba na Yanga.

STORI: LUNYAMADZO MLYUKA,Dar es Salaam

Chanzo: globalpublishers.co.tz