Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Coastal mechi ya  ubingwa 

844836bc92c5eadc03fc9b0ca8cd68e5.jpeg Simba, Coastal mechi ya  ubingwa 

Sun, 11 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

VINARA wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara Simba leo huenda wakatangazwa mabingwa rasmi ikiwa watashinda ama kupata sare dhidi ya Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Benjamini, Mkapa.

Simba inahitaji pointi moja pekee kutawazwa mabingwa hivyo, kama ikitoka sare itafikisha pointi 77 au kushinda itakuwa na pointi 79 na michezo miwili mkononi na kutawazwa mabingwa kwa mara ya nne mfululizo.

Pointi itakazofikisha Simba kwa matokeo hayo haziwezi kufikiwa na mtani wake wa jadi Yanga inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 70 ambaye kama atashinda mechi zake mbili zilizobaki atakuwa na pointi 76.

Taji la nne kwa wekundu hao wa Msimbazi litakuwa ni rekodi mpya kwa miaka ya karibuni kwani mara ya mwisho walichukua mara tano mfululizo kuanzia mwaka 1976-1980 na baada ya hapo walichukua mara tatu mfululizo mwaka 1993-1995 .

Mechi hiyo sio tu ina umuhimu kwa mabingwa hao watetezi bali kwa wageni wao Coastal Union ambao wako nafasi ya pili kutoka mwisho wakiwa wanapumulia mashine katika ukanda wa kushuka daraja.

Simba baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Yanga bao 1-0, mchezo uliofuata dhidi ya KMC walishinda mabao 2-0 na kurudisha morali yao.

Kiufundi Simba inaweza kushinda mchezo huo kutokana na ubora wake katika safu zote ikiwa na wachezaji wengi wenye kasi na uchu wa kutupia mabao kama John Bocco, Chris Mugalu, Luis Miquissone na Clatous Chama ikiwa wataendeleza moto wao.

Lakini hawapaswi kuwabeza Coastal kwasababu licha ya ubovu walionao wanaweza kuja kivingine na kuwapa upinzani kwani wanataka matokeo mazuri kujiondoa hatarini waliko.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana katika mechi ya mzunguko wa kwanza mkoani Arusha na Simba ilitoa kipigo kizito cha mabao 7-0, timu pekee iliyofungwa mabao mengi katika mchezo mmoja msimu huu.

Kocha wa Coastal Union Juma Mgunda atakuwa na kibarua kizito cha kuhakikisha anakuja na mbinu mpya kuzuia mashambulizi ya Simba, la sivyo, wanaweza kuchezea tena mvua ya mabao.

Katika michezo miwili iliyopita ya Coastal ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Tanzania Prisons na kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City na kushika nafasi ya 17 kwa pointi 34 katika michezo 31.

Chanzo: www.habarileo.co.tz