Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Azam zatembeza ubabe Taifa

81487 Simba+pic Simba, Azam zatembeza ubabe Taifa

Thu, 24 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Licha ya Simba kupata pointi tatu, mchezo dhidi yao na Azam FC uliochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana ulitawaliwa na ubabe.

Bao la Simba lilifungwa na Meddie Kagere katika dakika ya 49 kwa mpira wa kichwa akiunganisha krosi ya Fransis Kahata. Timu hiyo ilishinda kwa bao 1-0.

Hata hivyo, mwamuzi Hans Mabena kutoka Tanga alipata wakati mgumu kutokana na kusimamisha mpira mara kwa mara kufuatia wachezaji wa timu hizo kuchezeana rafu hasa kipindi cha kwanza.

Katika kipindi hicho walionyeshana ubabe jambo lililomlazimu Mabena kumpa kadi ya njano Frank Domayo, baada ya kumchezea rafu Hassan Dilunga dakika ya 14.

Dilunga aliyekuwa mwiba kwa Azam FC, alipunguzwa kasi mara kwa mara na idadi kubwa ya viungo wa timu hiyo walioongozwa na Mudathir Yahya na Domayo.

Ubabe wa timu hizo uliendelea na dakika ya 37 Kagere alionywa kwa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya beki Daniel Amoah.

Pia Soma

Advertisement
Kadi ya njano haikumuacha salama Amoah kwani naye alipewa na mwamuzi katika dakika ya 41 kwa kumchezea rafu Dilunga aliyekuwa jirani na lango la Azam.

Tukio hilo lilisababisha mchezo kusimama kwa dakika chache baada ya kutokea vurugu kwa baadhi ya wachezaji wa pande hizo kutaka kupigana kabla ya kusuluhishwa.

Dakika tatu baadaye mshambuliaji wa Azam FC, Obrey Chirwa alipewa kadi ya njano kwa kumkwatua kiungo wa Simba, Muzamiru Yassin.

Katika mchezo huo, Simba ilianza na viungo wanne - Gerson Fraga, Hassan Dilunga, Mzamiru na Kahata.

Pia Azam FC iliwatumia wanne ambao Mudathir Yahya, Joseph Mahundi, Frank Domayo na Salum Abubakari ambao walionyeshana ufundi katika eneo la katikati ya uwanja.

Sharaf Shiboub ambaye ni kiungo alicheza eneo la ushambuliaji, lakini mara kwa mara alirudi katikati kuwakabili Domayo na Mudathir kabla ya kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Clatous Chama.

Rekodi

Rekodi zinaonyesha Simba imekuwa ikifanya vizuri dhidi ya Azam FC pindi timu hizo zinapokutana kwenye Ligi Kuu na wameibuka na ushindi mara nyingi kuliko wapinzani wao. Katika matokeo ya mechi 11 zilizopita baina yao, Simba imeshinda mara tano, Azam FC mara moja na zimetoka sare mechi tano.

Azam FC haijapata ushindi dhidi ya Simba kwa siku 997 katika mechi za Ligi Kuu tangu iliposhinda Januari 28, 2017 kwa bao 1-0. Baada ya hapo ilifungwa mara mbili kati ya mechi nne na kutoka sare mechi mbili. Katika mechi za msimu uliopita Simba ilishinda mabao 3-1 Februari 22 kabla ya kutoka suluhu Mei 13, mwaka huu.

Simba: Aishi Manula, Haruna Shamte, Gadiel Michael, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Gerson Fraga, Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Shaaraf Shiboub na Francis Kahata.

Azam FC: Mwadini Ally, Nicolaus Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Daniel Amoah, Mudathir Yahya, Joseph Mahundi, Frank Domayo, Obrey Chirwa, Richard Djodi na Salum Abubakar.

Mechi nyingine, Prisons ilitoka suluhu na Biashara United, Alliance iliichapa Ruvu Shooting 1-0, Namuongo iliichakaza Mtibwa Sugar 1-0, Polisi Tanzania iliichapa Mwadui 1-0, Coastal Union ilitoka suluhu na Singida United, Ndanda ilipata sare ya 1-1 dhidi ya Lipuli.

Chanzo: mwananchi.co.tz