Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Azam vita ya Majimaji leo

Simba SAFI Simba, Azam vita ya Majimaji leo

Sat, 26 Jun 2021 Chanzo: ippmedia.com

Utakuwa mchezo mgumu kwa pande zote mbili, kwani kila wanapopambana, mechi itakuwa kali, na ya kusisimua kwa mashabiki walio uwanjani na wanaofuatilia kwenye televisheni na redio.

Wakati Simba ikionekana kama kutaka kwenda fainali ikilitaka kombe hilo kwa ajili ya heshima na kulitetea, Azam inaonekana kulitaka kwa udi na uvumba kwani ndiyo safari ya uhakika zaidi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Kocha Mkuu wa Simba Didier Gomes amekiri kuwa watakuwa na kibarua kizito kucheza dhidi ya Azam FC kwani timu moja kati ya timu nzuri nchini.

"Utakuwa mchezo mgumu. Tunawaheshimu Azam kwa sababu tunajua uwezo wao, lakini sisi tumejipanga kufika fainali. Tunataka kushinda makombe yote, Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho," alisema kocha huyo.  

Alisema kwenye mchezo huo ni lazima wachezaji wake wacheze kwa kujituma na kuonyesha uwezo kama wanataka kufika fainali kwani malengo yao ni kushinda kombe hilo pia.

Nahodha wa timu hiyo, John Bocco ambaye anakwenda kukutana na waajiri wake wa zamani, alisema wanakwenda kukutana na timu nzuri na ngumu, lakini wao wamejipanga na Mungu atawasaidia.

"Tunakwenda kukutana na timu nzuri. Tunawaheshimu kwa hilo, lakini tumejipanga, Mungu atatusaidia kupata matokeo mazuri na kufuzu fainali." Alisema Bocco.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati, amesema mechi itakuwa ngumu kwa sababu ni timu moja tu inayotakiwa kuingia fainali.

"Tunaelewa umuhimu wa mechi. Tutapambana, haitokuwa kazi rahisi, lakini hatutowaangusha mashabiki wetu kwa sababu nia yetu kwenye kusaka nafasi ya kwenda fainali," alisema Bahati.

Chanzo: ippmedia.com