Dar es Salaam. Kocha wa mpya wa Azam, Hans Pluijm na mpinzani wake Masoud Djuma wa Simba wote wanasifika kwa kucheza soka la kushambulia na pasi nyingi.
Uwezo wa makocha hao katika kutegeneza mashambulizi umezifanya Simba na Azam kukutana kwa mara ya kwanza katika fainali ya Kombe la Kagame.
Kocha Pluijm ni muumini wa mfumo 3-5-2, 4-4-2 na 4-3-3 atakuwa na kibarua kigumu mbele ya Masoud naye amekuwa ni mzuri wa kutumia mfumo 3-5-2 na 4-3-3 jambo linalofanya mchezo huo wa fainali utachezwa zaidi katikati ya uwanja.
Mdachi huyo ataendelea kuwatumia viungo wake Frank Domayo, Salum Abobakari ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya, Joseph Mahundi na Ramadhani Singano wataonyeshana kazi wenzao wa Simba ambao ni Mwinyi Kazimoto, Muzamiru Yassin, James Kotei, Mohamed Rashid.
Katika kuhakikisha Simba hawapati nafasi ya kufanya mshambulizi yao kutokea pembeni Pluijm ataendelea kuwatumia Bruce Kangwa na Nicco Wadada wakati Mrundi Masoud atawapa jukumu Nicholaus Gyan na Mohammed Hussen ‘Zimbwe’.
Kutokana na mfumo wa timu hizo mbili hakuna shaka kwamba mchezo huo utamalizika ndani ya dakika 90, kwa makosa madogo madogo ya wachezaji mmoja moja yanaweza kubadilisha matokeo.
Hata hivyo, Pluijm anakwenda kwenye mchezo huo akiwa na rekodi mbaya dhidi ya Simba msimu uliopita baada ya kupoteza mechi zote mbili za Ligi Kuu akiwa na Singida United, lakini wakati huo mabingwa hao wa Ligi Kuu wakiwa chini ya kocha Mfaransa Pierre Lechantre akisawaidiwa Masoud.
Timu hizo ambazo zimekutana mara nne katika hatua za fainali za mashindano mbalimbali zinatarajia kuchoshana nguvu na kila mmoja kuamua nani mbabe wa mwenzake katika kombe hilo.
Kwa mujibu wa rekodi zinaonyesha hakuna mbabe wa mwenzake katika makombe hao kutokana na kila mmoja kushinda mara mbili kati ya mara nne walivyokutana.
Msimu wa mwaka 2012 Azam waliibuka na ushindi wa bao 3-1 dhidi ya Simba katika hatua ya robo fainali mashindano ya kombe la Kagame, msimu huo huo Azam aliendeleza ubabe wake kwa kumtoa Simba katika hatua ya nusu fainali kombe la mapinduzi baada ya ndani ya dakika tisini kuchoshana nguvu kwa kufungana bao 2-2(Azam akashinda kwa penalti 5-4).
Msimu huo huo wakakutana tena kuwania Kombe la Urafiki ambapo walikutana katika hatua ya fainali Azam alikubali kichapo cha mabao 1-3 kutoka Simba kutwaa ubingwa huo, Simba aliendeleza ubabe tena katika mashindano ya Kombe la Benki ABC Azam FC alikubali kipigo cha mabao 2-1.