Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Azam patachimbika

97930 Pic+azam.png Simba, Azam patachimbika

Sat, 30 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ni katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la FA, 'dabi' nyingine yanukia karibuni...

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba watakutana na Azam FC katika mechi ya hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la FA wakati watani zao, Yanga wataikaribisha Kagera Sugar.

Mechi hizo za hatua ya robo fainali ya mashindano hayo ambayo hutoa tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, zimepangwa kufanyika kati ya Juni 27 na 28, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Awali kabla ya kutokea kwa janga la ugonjwa wa corona (COVID 19), fainali za michuano hiyo ambayo bingwa mtetezi ni Azam FC, ilipangwa kufanyika Mei 30, mwaka huu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mkoani Rukwa.

Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano hayo iliyopangwa jana, endapo vigogo hao wa soka nchini watasonga mbele, basi watakutana kwenye hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo.

Akizungumza baada ya ratiba hiyo kutoka, Mwakilishi wa Simba, Khamis Kisiwa, alisema nia ya timu yake ni kupambana na hatimaye kuchukua kikombe cha mashindano hayo.

"Nia na madhumuni ni kuchukua kikombe, sio hiki, hata hicho ambacho wanafikiri tutalegezalegeza, nia yetu ni kuchukua vikombe vyote viwili," alisisitiza Kisiwa.

Aliongeza katika mchezo uliopita, walipanga kupata ushindi kwa penalti lakini sasa wataingia tofauti zaidi.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat', alisema mechi hiyo itakuwa na ushindani wa pande zote mbili na hatuna timu ndogo kati ya hizo mbili.

"Ni robo fainali nzuri, inakutanisha mkubwa na mkubwa mwenzie, kwa sababu wote sisi ni wakubwa, mechi zetu zote na Simba zimekuwa na ushindani, itakuwa mechi nzuri, lakini kila mmoja atapambana ili aweze kwenda kuchukua kikombe hiki," Popat alisema.

Popat alisema nguvu zao zote wameziweka kwenye mashindano ya Kombe la FA baada ya kuona nafasi yao ni finyu kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Mechi nyingine za hatua ya robo fainali ya michuano hiyo itakuwa ni kati ya Namungo FC ya Lindi dhidi ya Alliance FC kutoka jijini Mwanza wakati Sahare All Stars ya Tanga itapambana na Ndanda FC ya Mtwara.

Meneja Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, alisema jana timu zote nane zinatakiwa kujiandaa vema kuelekea michezo hiyo kwa sababu hatua waliyofika ina ushindani zaidi.

Kizuguto alisema shindano hili limeendelea kuwa na ubora wa hali ya juu na timu mbalimbali zimefanikiwa kushinda kombe la mashindano haya.

"Timu tunaziomba zijiandae, ziwe tayari na mashindano haya, yoyote atakayekuwa amejiandaa atafanya vizuri, kama TFF tumejiandaa kucheza kwa kufuata mwongozo ambao tunausubiri, hatua hii si nyepesi, hatua hii si ndogo, mshindi wa mashindano haya ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa," alisema Kizuguto.

Aliongeza mechi za mashindano hayo zitakuwa nyumbani na ugenini, lakini hii itatangazwa baada ya kupata mwongozo rasmi kutoka kwa idara husika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live