Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Azam ni kisasi

Fa910079f907e0588659a609cbfa7315 Simba, Azam ni kisasi

Sat, 26 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KOCHA Mkuu wa Simba, Didier Gomes anakabiliwa na kibarua kizito wakati kikosi chake kitakapokutana dhidi ya Azam FC, katika mchezo wa nusu fainali wa Kombe la FA utakaopigwa jioni ya leo Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Simba ndio bingwa mtetezi wa taji hilo baada ya kulitwaa msimu uliopita kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Namungo FC, hivyo haitokuwa mechi rahisi kwa Gomes, ambaye amelikuta taji hilo hasa kutokana na ubora waliokuwa nao Azam ukichangia na kupoteza matumaini ya ubingwa wa ligi.

Simba imefika hatua hiyo, baada ya kuifunga Kagera Sugar mabao 2-1 Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam wakati Azam FC ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Rhino Rangars iliyopo Daraja la Pili.

Kutokana na ubora wa pande zote mbili ni vigumu kutabiri mshindi wa mchezo huo, kwani hata kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi, timu hizo zilipokutana ziligawana pointi kwa kufungana mabao 2-2.

Simba ambao ndio wenyeji wametamba wakisema pamoja na ubora wa kikosi cha Azam, lakini watashinda mchezo huo kutokana na ubora wa kikosi chao, lakini ari waliyokuwa nayo ya kutaka kuwa timu ya kwanza kutwaa taji hilo mara mbili mfululizo.

Kocha Gomes alisema anaimani kubwa sana na jeshi lake na hiyo ni kutokana na kuimarika katika kila mechi waliyocheza hivyo haoni kama wapinzani wao Azam wanaweza kumzuia asiingie kwenye historia ya kuwa miongoni mwa makocha walioiongoza timu hiyo kubeba taji hilo.

“Ni mchezo mkubwa sababu umepewa jina la nusu fainali, kitu kizuri kwangu sina hofu na wachezaji wangu naamini wanafanya kazi yao kwa ukamilifu na baada ya dakika 90 Simba itashinda, natambua ubora waliokuwa nao Azam, lakini wanapaswa kujua Simba ni bora zaidi yao,” alisema Gomes.

Kocha huyo raia wa Ufaransa amesafiri na nyota wake wote ispokuwa kiungo Jonas Mkude aliyesimamishwa na uongozi kutokana na utovu wa nidhamu lakini kocha huyo alisema kukosekana kwake hakuwezi kuigharimu timu yake kupata ushindi.

Gomes ambaye hivi karibuni timu yake imekuwa ikitoa vipigo takatifu kwa wapinzani katika nafasi ya kipa anatarajiwa kumwanzisha kipa Aishi Manula ambaye alikosekana kwenye mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Mbeya City kutokana na kuwa na kadi tatu za njano.

Nyota wengine wanaotarajiwa kuanza kikosi cha kwanza leo ni nahodha John Bocco atakayeongoza mashambulizi akisaidiwa na Luis Miquissone, Cletus Chama aliyerejea dimbani mechi iliyopita, huku kwenye eneo la kiungo akitarajiwa kuwaanzisha Taddeo Lwanda, Erasto Nyoni au Mzamiru Yassin.

Kwaupande wake kocha msaidizi wa Simba Vivier Bahati, amekiri mchezo huo utakuwa mgumu sababu ni mchezo mmoja na atakayefungwa anatoka lakini wamekiandaa kikosi chao kwa ajili ya kupata ushindi bila kujali ubora walionao wapinzani wao Simba.

Bahati alisema hawatishwi na mapokezi makubwa waliyoyapata Simba sababu hicho nikitu cha kawaida hata kama wangecheza Azam Complex mashabiki ambao wangejaza uwanja wangekuwa wakwao ispokuwa wamewaanda wachezaji wao kiakili na kucheza kimbinu ili kushinda.

“Tumekuja na kikosi kamili akiwemo Prince Dube, ambaye hatukumtumia kwenye mechi mbili zilizopita dhidi ya Gwambina na Namungo lakini pia wachezaji wetu wote wapo sawa kwa ajili ya mchezo huo tumejipanga kuhakikisha tunacheza kwa nidhamu ili kupata ushindi,” alisema Bahati.

Ukimtoa Dube mshambuliaji Mpiana Monziz raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo huenda akatumika katika mchezo huo kama msaidizi wa Dube, baada ya kiwango alichokionesha kumvutia kocha George Lwandamina ikiwemo mabao mawili aliyofunga dhidi ya Gwambina.

Ushindani katika mchezo hou unatarajiwa kuwa mkali kwenye eneo la kiungo kutokana na timu zote mbili kutumia mfumo unaofanana wa kujaza viungo wengi na kucheza mpira wa pasi nyingi.

Mshindi katika mchezo huo atacheza fainali dhidi ya Yanga ambayo jana ilishinda kwa tabu 1-0 dhidi ya Biashara United kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Chanzo: www.habarileo.co.tz