Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siku 897 za Jamal Malinzi nje ya soka

88174 Pic+malinzi Siku 897 za Jamal Malinzi nje ya soka

Sat, 14 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya kukaa siku 897 mahabusu, hatimaye rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na aliyekuwa katibu wake Celestine Mwesigwa jana walikwepa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kukubali kulipa faini ya Sh500,000 kutokana na kosa la kughushi nyaraka.

Licha ya kukwepa kwenda jela, Malinzi hataweza kurejea tena katika ulingo wa soka baada ya kufungiwa kwa miaka 10 na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).

Hiyo inamaanisha kuwa hata kama atataka tena kurudi kuongoza mpira wa miguu katika ngazi yoyote anatakiwa kuilipa Fifa faini ya Dola 503,000.

Novemba 11, mwaka huu, Fifa ilimfungia Malinzi miaka 10 kwa kosa la kupokea Dola 528,000 ikiwa ni mkopo wa miaka minne alipokuwa madarakani, lakini alishindwa kutoa taarifa sahihi ya matumizi ya fedha hizo.

Malinzi anatuhumiwa pia na Fifa kupokea Dola 55,000 - fedha ambazo zilikuwa zawadi kwa timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya miaka 17 kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2017 nchini Gabon.

Kwa mujibu wa Fifa, Malinzi aliyekuwa mjumbe wa kamati ya maendeleo alikuwa akitoa fedha katika miradi yote duniani wakati alipokuwa katika jukumu hilo kuanzia 2013-2017 ndipo alipochukua fedha hizo. Malinzi pia anatakiwa kulipa faini ya Dola 503,000 kwa Fifa.

Katika kesi iliyokuwa ikimkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Malinzi alihukumiwa kwenda jela au kulipa faini baada ya kukutwa na kosa hilo ambapo katika shtaka la tatu kati ya mashtaka yaliyokuwa yanamkabili ilielezwa kuwa alitengeneza nyaraka inayoeleza kikao cha kamati tendaji ya TFF kilibadili watia saini.

Mwesigwa kwa upande wake atatakiwa kulipa faini ya Sh1,000,000 baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili ya kutengeneza nyaraka ya uongo na kuitumia. Hata hivyo, jana washtakiwa wote walirudishwa gerezani baada ya kushindwa kukamilisha utaratibu wa malipo ambapo wanatakiwa kulipia benki.

Malinzi na Mwesigwa walikamatwa Juni 27, 2017 na kupandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Juni 29 pamoja na aliyekuwa mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga wakikabiliwa na mashtaka 28 ikiwamo ya kughushi na kutakatisha Dola za Marekani 375,418.

Hata hivyo jana, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu chini ya Hakimu Mkazi Maira Kasonde iliwakuta na hatia ya mashtaka ya kughushi Malinzi na Mwesigwa, hivyo kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini huku ikiwaachia huru Nsiande na aliyekuwa karani wa TFF, Mariam baada yakuwakuta hawana hatia.

Malinzi aliiongoza TFF kuanzia Oktoba 2013 ambapo alikaa madarakani hadi Juni 2017 alipokamatwa kwa tuhuma za utakatishaji fedha ndani ya shirikisho hilo.

Licha ya kukamatwa na kushtakiwa mwenyekiti huyo wa zamani wa Chama cha Soka Mkoa wa Kagera, hakukata tamaa kwani wakati wa kinyang’anyiro cha uchaguzi kuwania awamu ya pili ya uongozi wa TFF mwaka 2017 alijitosa tena kutaka kutetea nafasi yake ya urais kabla ya jina lake halijakatwa kwa kushindwa kufika kwenye usaili wakati huo alikuwa rumande akikabiliwa na kesi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi TFF wa wakati huo, Revocatus Kuuli alisema mgombea ambaye atakosa kufika kwenye usaili katika muda huo atakuwa amejiondoa, hivyo hadi uchaguzi ulipomalizika Wallace Karia alishinda na kuwa rais mpya wa TFF mpaka sasa.

Chanzo: mwananchi.co.tz