Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yashauri Yanga kuisapoti Simba Afrika

34374 Pic+simba Tanzania Web Photo

Tue, 1 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali imeahidi kuisapoti Simba kwa hali na mali kwenye mechi zake za Ligi ya Mabingwa Afrika huku ikiwaomba mashabiki wa Yanga kuwaunga mkono wenzao wa Simba watakapocheza mechi za nyumbani kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba ambayo imetinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, itacheza mechi tatu nyumbani na ugenini dhidi ya Al Ahly ya Misri, JS Saoura (Algeria) na AS Vita ya DR Congo.

Akizungumza katika mahojiano mafupi na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo alisema Serikali ina mpango wa kuzungumza na uongozi na mashabiki wa Yanga ili kuondoa tofauti zao na Simba kwenye mechi za kimataifa kuanzia mwaka huu.

Pamoja na kwamba ni ngumu kwa mashabiki wa pande zote mbili, lakini Serikali imepanga kutoa semina kwa mashabiki wa timu hizo kuhusu uzalendo endapo mmoja wapo anacheza kimataifa na itaanza na Yanga.

“Unajua ni fedheha kwa nchi eti timu ya kwetu inacheza, lakini mashabiki wa nchi yetu baadhi wanaiunga mkono, tunahitaji kubadilika mwaka 2019,” alisema Singo.

Alisema kama Serikali inafikiria kuzungumza na mashabiki na wanachama wa Yanga ili waisapoti Simba kwenye mechi zake za nyumbani za Ligi ya Mabingwa zitakazoanza mapema mwezi huu.

“Utani wa Simba na Yanga unastahili, lakini tujaribu kuuweka kwenye mechi za kitaifa, tutakutana na watu wa Yanga, tutazungumza nao na kuwaomba waisapoti Simba, lakini pia hata ikitokea Yanga wanacheza kimataifa, basi wapate sapoti ya Simba, utani wao ubaki kwenye mechi zetu za humu humu.

“Tutapeana elimu ya kizalendo na mashabiki wa pande zote mbili, ili tuondoe fikra kuwa Al Ahly wakija kucheza na Simba, mashabiki wa Yanga wanaisapoti, hii si sawasawa,” alisema.

Akizungumzia sapoti ya Serikali kwa Simba, Singo alisema wengi wanahitaji kuona wakitoa fedha katika sapoti hiyo, lakini watafanya hivyo endapo Simba itaomba na wao wataangalia ni namna gani wataisaidia.

“Mbali na fedha, sapoti nyingine tutakayoitoa ni kuwawekea mazingira mazuri kwenye nchi Simba watakayokwenda kucheza, ikiwamo kuongea na balozi zetu kwenye nchi hizo ili kuifanya timu iwe salama zaidi hadi inarejea,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz