Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yapigilia msumari uwekezaji Simba, Yanga

68191 Uwekezaji+pic

Thu, 25 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali imetoa mwongozo wa mfumo wa uendeshaji wa klabu za soka nchini, zilizoanzishwa na wananchi ambako asilimia 49 ya hisa anazopewa mwekezaji hazipaswi kuhodhiwa na mtu mmoja.

Miezi kadhaa iliyopita Serikali ilibadili kanuni kwa kuruhusu uendeshaji wa hisa kwenye klabu za wanachama kumpa mwekezaji asilimia 49 na 51 kubaki kwa wanachama.

Klabu ya Simba ilikuwa ya kwanza kubadili mfumo wa uendeshaji kwa kumpa asilimia 49 mfanyabiashara maarufu nchini Mohammed Dewji ‘Mo’ na wanachama kubaki na 51.

Hata hivyo, jana Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk Harrison Mwakyembe katika mkutano wake na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), alisema asilimia 49 ya hisa hazipaswi kuhodhiwa na mwekezaji mmoja.

“Kazi ya kuweka utaratibu gani wa asilimia 49 tuliiachia TFF ifanye kwa mujibu wa kanuni, lakini kazi haikufanyika mpaka sasa (jana mchana),” alisema Dk Mwakyembe.

Alisema hawezi kuwalaumu TFF, lakini wamekubaliana kanuni zifanyiwe marekebisho ili kuboresha usimamizi huo wa hisa na wajibu huo ubaki kwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na si TFF.

Pia Soma

“Nimeshauri iundwe kamati ndogo ya wataalamu kuweka kanuni vizuri ambapo katika kamati hiyo kutakuwa na mjumbe mmoja kutoka BMT, TFF, kurugenzi ya michezo, mwakilishi wa wadau, TRA na wajumbe wawili kutoka soko la hisa na mitaji,” alisema.

Awali, katika mchakato huo kwa Simba, Dewji alitaka asilimia 51 ya hisa na wanachama kubaki na 49 kabla ya Serikali kuingilia kati na kupitisha wanachama kubaki na asilimia 51 na mfanyabiashara huyo kupewa asilimia 49.

Kauli ya Simba

Wakati Dk Mwakyembe akitoa agizo hilo, Mjumbe wa Bodi ya Simba ambaye aliongoza mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema hana taarifa ya suala hilo.

“Litatakapofika mezani kwetu tutatafakari kwanza na kama wawekezaji wengine watakuwepo na kujitokeza sawa, ila likitufikia tutatangaza wakikosekana basi,”alisema Try Again ambaye aliwahi kuwa kaimu rais wa klabu hiyo.

Mwanasheria, Alex Mgongolwa alisema kwa kuwa agizo limetolewa na Serikali, klabu zinazoelekea katika mfumo huo zinatakiwa kufuata. “Klabu zinasajiliwa kwa mujibu wa sheria ni jambo la kawaida sheria itakapobadilishwa lazima ufuate kwani zinafanya kazi kwa misingi ya sheria kwa kuwa wakati zinasajiliwa zilisema zitafuata sheria, hivyo hakuna cha ajabu zaidi ya kufuata Serikali inavyotaka,” alisema Mgongolwa.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Simba, Hamisi Kilomoni alisema amepokea vyema tamko hilo akisisitiza kinachotakiwa ni klabu kufuata sheria.

Chanzo: mwananchi.co.tz