Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yapewa mbinu kukuza Vipaji mashuleni

Kaijage Michezo Serikali yapewa mbinu kukuza Vipaji mashuleni

Fri, 3 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha mstaafu wa timu ya taifa (Taifa Stars) na mkufunzi wa makocha nchini, Rogasian Kaijage amesema ili michezo ikue shuleni na kuzalisha wanafunzi wenye vipaji vikubwa, Serikali inapaswa kuifanya fani hiyo kuwa sehemu ya mtaala ili kuwabana walimu kuutekeleza.

Amesema shule zote nchini zinapaswa kuwa na miundombinu ya michezo, vifaa na walimu ili kuwafanya wanafunzi kupata msingi mzuri wa michezo wakiwa shule za msingi na watakapofika sekondari wachague aina ya michezo watakayopenda kujiendeleza nayo.

Kaijage ametoa kauli hiyo Machi 2, 2023 jijini Mwanza wakati taasisi yake ya Sport Charity ikikabidhi mipira zaidi ya 400 kwa shule za msingi, sekondari na vituo vya michezo wilayani Nyamagana hafla ambayo imefanyika katika viwanja vya Mirongo.

“Tuweke nguvu kuhakikisha kila shule inajihusisha na mchezo na ina walimu ili watoto waanze kuipenda fani hii wakiwa shuleni na iwe kwenye mtaala na siyo kitu cha nyongeza tu ili iwabane walimu waifuate, tunataka tuzifanye shule ziwe academy za awali zikiwa na mahitaji muhimu wanafunzi wapate msingi wakiwa ngazi ya awali,”

“Mpango huu ni kwa shule zote mkoa wa Mwanza leo tumetoa kwa shule 145 za msingi na 60 za sekondari na vitalu vya Umiseta na Umitashumta, tulianza programu hii na klabu za soka za Mwanza mabadiliko tunaanza kuyaona timu zinafanya mazoezi zikiwa na vifaa,” amesema Kaijage.

Kaijage amesema taasisi yake itaendelea kusaidia kukuza michezo nchini kwa kujenga miundombinu, kununua vifaa vya michezo ili kusaidia kuandaa timu kujenga wana michezo kwenye soka, netiboli, wavu, kikapu, kriketi na mpira wa mikono.

Naye, Naibu Meya jiji la Mwanza, Bhiku Kohotecha amepongeza juhudi za taasisi hiyo katika kuisaidia Serikali kuinua michezo kwa kujenga miundombinu na kutoa vifaa huku akiiomba kuendelea kutoa msaada huo kwani miongoni mwa wanafunzi wanaonufaika na vifaa hivyo watakuwa wanamichezo wakubwa baadaye.

Kaimu Mkurugenzi jiji la Mwanza, Msingo Maisa amempongeza Kaijage kwa kusaidia kutatua changamoto ya miundmbinu na vifaa kwenye shule huku akiwataka wazazi na jamii kuwashirikisha watoto kwa bidii katika michezo ambapo amewataka walimu kutunza vifaa hivyo na kuvitumia kwa lengo lililokusudiwa.

Mwalimu wa mchezo wa kikapu shule ya msingi Nyakabungo, Haidari Abdul, amesema msaada huo utawasaidia kuzalisha watoto wengi wanaopenda mchezo huo katika kitalu chao cha mchezo wa kikapu chenye wanafunzi zaidi ya 50 kuanzia darasa la pili hadi la tano.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live