Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yanasa wanane waleta vurugu Yanga

32544 Yanga+pic Tanzania Web Photo

Thu, 20 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo amesema wamekaa vikao vingi na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraza la Michezo Tanzania (BMT), viongozi wa Yanga pamoja na wawakilishi wa Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo.

Singo alisema vikao hivyo vyote vilikuwa ni kutafuta mwafaka wa klabu ya Yanga kufanya uchaguzi na kupata viongozi wapya.

Anasema wakati hayo yakiendelea Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alipokea majina ya watu nane ambao wanafanya vikao vya kimyakimya ili kuvuruga uchaguzi.

“Serikali chini ya Waziri, majina hayo tunayo ambayo wanafanya vikao ambavyo si rasmi ili kuchochea uchaguzi wa Yanga usifanyike,” alisema.

“Waziri leo (Jana) asubuhi amechukua majina hayo ya watu nane ambayo ameyapeleka katika vyombo husika ili kufanyiwa uchunguzi na endapo watabainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

“Waziri alisema hao ambao wanapinga uchaguzi wa Yanga usifanyike kama ulivyopangwa ni wale ambao wanakataa kujiuzuru kwa Yusuf Manji,” alisema.

Singo aliwataja wahusika hao kuwa ni Mustapha Mohamed, Edwin Kaisi, Said Bakari, Shaaban Omary, Kitwana Kondo, Boazi Ikupilika, Bakili Makere na David Sanare. Hata hivyo Makere alishafungiwa kujihusisha na masuala ya michezo kwa miaka mitatu.

Mmoja ya wanachama ambaye anashtumiwa, Kaisi Edwin alisema Waziri amepelekewa majina yao lakini wao si watu wanaopinga mchakato wa uchaguzi wa Yanga.

Alisema: “Si kama tunapinga uchaguzi, tunachokataa uchaguzi wetu kusimamiwa na TFF wakati Katiba ya Yanga na hata TFF hairuhusu uchaguzi wetu kusimamiwa na wao.

“Huo ndio msimamo wetu na hatutarudi nyuma wala kuzibwa mdomo katika hili, na kwa kuwa wameenda huko na sisi tutafika katika vyombo husika ili kupata tafsiri ya sheria.”



Chanzo: mwananchi.co.tz