Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali: Tulikuwa na nia njema kusogeza mechi

A008ba7f0604c497885556a9ed827173.jpeg Serikali: Tulikuwa na nia njema kusogeza mechi

Wed, 12 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imewaomba viongozi wa Simba, Yanga na mashabiki kuwa watulivu katika kipindi hiki na kuamini ilikuwa na nia njema na sababu za msingi iliposhauri awali mchezo huo usogezwe mbele kwa saa chache.

Hivyo imesema mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utarudiwa na mashabiki waliokata tiketi watarejeshewa tiketi zao kwa ajili ya kutazama mchezo ujao.

Serikali imeamua hivyo baada ya mchezo huo uliopangwa kufanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kuahirishwa.

Mchezo huo uliokuwa uchezwe saa 11 jioni kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam ulisogezwa mbele mpaka saa moja jioni ambapo kwa mujibu wa TFF ilisema ilipata maelekezo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Taharuki ilianzia hapo kwani Yanga ilipeleka timu uwanjani kucheza saa 11 na Simba ilipeleka timu kucheza saa moja kabla mamlaka zinasosimamia soka hazijatangaza kuahirisha mechi hiyo.

Katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, John Mapepele kwa vyombo vya habari jana, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa alifanya kikao na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) Bodi ya Ligi (TPLB), Baraza la Michezo (BMT), Simba na Yanga na kufikia muafaka.

“Serikali imeagiza mchezo wa Simba na Yanga ambao ulikuwa uchezwe Jumamosi iliyopita urudiwe hivyo TPLB na TFF wapange siku ya kuchezwa mchezo na fedha za mashabiki waliolipa kituo cha kitaifa cha data kuwarejeshea tiketi mashabiki wote 43,947 waliokuwa wamekata tiketi na watumie tiketi hizo kuangalia mchezo mwingine...

“Mashabiki ambao walikuwa hawajakata tiketi waruhusiwe kukata tiketi zilizobaki kulingana na uwezo wa Uwanja wa Benjamin Mkapa,” ilisema taarifa hiyo.

Pia Waziri ameahidi kuitisha kikao haraka kati ya TFF na Yanga ili kujadili tofauti zilizopo kuondoa mgongano baina ya pande hizo mbili, tarehe za kikao hicho itapangwa katika siku za karibuni.

Aidha Waziri amerejea kuwaomba radhi mashabiki na wapenzi wa soka kufuatia kusogezwa mbele kwa saa kadhaa na baadaye kuahirishwa kwa mechi hiyo.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara, Dk Hassan Abbasi, Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Neema Msitha, Rais wa TFF, Wallace Karia na Katibu wake Mkuu, Kidao Wilfred, Mwenyekiti wa TPBL, Stephen Mguto na Mtendaji wake Almas Kasongo.

Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, Mtendaji Mkuu Arbara Gonzalez, Mjumbe wa Bodi ya Simba, Zacharia Hanspope, Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla, Mjumbe wa kamati ya utendaji Yanga, Bahati Mweseba na Kaimu Katibu Mkuu Yanga, Haji Mfikirwa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz