Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serengeti Boys ndio hivyo, kama mlivyosikia

13799 Pic+serengeti TanzaniaWeb

Sat, 25 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Timu za vijana za Uganda na Ethiopia jana zilijikatia tiketi ya kutinga fainali ya michuano ya kufuzu kwa fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 17.

Uganda ilitinga fainali baada ya kushinda mechi ya pili ya nusu fainali dhidi ya Tanzania ‘Serengeti Boys’ kwa mabao 3-1, wakati katika nusu fainali ya kwanza Ethiopia ilikata tiketi kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya sare ya mabao 2-2 na Rwanda katika dakika 90 za mchezo.

Katika nusu fainali ya kwanza Rwanda iliyokuwa ikipewa nafasi kufika fainali ilipoteza penalti mbili huku Ethiopia ikipata penalti zote nne ilizopiga na hivyo kutinga fainali.

Katika nusu fainali ya pili, Uganda ilizima ndoto za Tanzania kuwa kuibandua mabao 3-1 katika mchezo ambao hata hivyo Serengeti Boys haikucheza mpira wake uliozoeleka.

Uganda ilikuwa ya kwanza kufanya mashambulizi ambayo yalizaa matunda baada ya kupata bao la kuongoza mapema dakika ya nne ya mchezo likifungwa na Abdulwahid Idd aliyeunganisha wavuni mpira wa kona baada ya kutokea piga nikupige.

Kuingia kwa bao hilo kuliipa nguvu safu ya ulinzi ya Uganda iliyojizatiti kuwadhibiti washambuliaji wa Serengeti Boys wasiweze kuleta madhara kwenye lango lao.

Hata hivyo katika dakika ya 11 Serengeti Boys, walichomoa bao hilo baada ya Edson Mshirakandi kupiga kona iliyokwenda moja kwa moja wavuni ikimuacha kipa wa Uganda, Oyo Delton akiruka bila mafanikio.

Kuingia kwa bao hilo kuliamsha hoihoi kwa mashabiki waliojitokeza uwanjani kuipa sapoti timu hiyo.

Makali ya safu ya ushambuliaji ya Serengeti Boys inayoongozwa na Agiri Ngoda na Kelvin John hayakuonekana katika mchezo wa jana, baada ya kubanwa vilivyo na mabekiwa Uganda.

Kipindi cha pili vijana wa Uganda walikianza kwa kasi kama walivyofanya kipindi cha kwanza wakijilinda zaidi na kufanya mashambulizi ya kushitukiza.

Mbinu hizo zilizaa matunda baada ya kupata bao la pili lililotokana na mpira wa adhabu ambao uligonga mwamba na walinzi wakachelewa kuuokoa ndipo John Alou akafunga kirahisi dakika ya 76.

Juhudi za vijana wa Serengeti Boys kusaka bao la kusawazisha zilishindikana na kadiri muda ulivyosonga ndivyo walivyozidi kupoteana wakipoteza mipira kirahisi na washambuliaji wake wakosa ushirikiano kila mmoja akitaka kufunga hata kama hayupo kwenye nafasi nzuri. Uganda ni kama walikuwa wameingia uwanjani kwa lengo la kuhakikisha mshambuliaji wa Serengeti, Kelvin John hapeleki madhara langoni mwao, lakini hata hivyo Serengeti walikuwa wakitumia njia nyingine ya kutumia mipira ya krosi katika kupeleka mashambulizi lakini mambo hayakuwa.

Jahazi la Serengeti Boys lilizama katika dakika ya 90 baada ya mlinzi Amiri Njiru kuuweka mpira wavuni alipojaribu kuokoa krosi iliyoelekezwa langoni mwake.

Kwa matokeo hayo, Serengeti italazimika kucheza na Rwanda mapema Jumapili kusaka mshindi wa tatu, kabla ya kuzipisha Ethiopia na Uganda katika fainali.

Chanzo: mwananchi.co.tz