Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serengeti Boys kufa au kupona kwa Uganda

52719 PIC+SERENGETI

Wed, 17 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki saa chache kabla ya kushuka uwanjani kuikabili timu ya Taifa ya vijana ya Uganda, Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo amesema mchezo huo utakuwa wa kufa au kupona.

Serengeti Boys leo inatupa karata yake ya pili katika mchezo wa Fainali ya Kombe la Mataifa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, baada ya kufungwa mabao 5-4 na Nigeria katika mechi ya ufunguzi.

Ushindi wa leo saa moja usiku, bila shaka utafufua matumaini ya Serengeti Boys kushinda mechi yake ya mwisho dhidi ya Angola ili kukata tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil, mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam jana, kocha huyo alisema kutokana na umuhimu wa mechi hiyo, vijana wake wameibuka na kauli mbiu ya ‘Do or Die’ ambayo wamekuwa wakiitumia kambini.

Mirambo alisema kauli mbiu hiyo imeongeza morali kwa wachezaji ambao kila mmoja ameahidi kucheza kwa nguvu endapo atapata nafasi ya dhidi ya Uganda.

Kocha huyo alisema katika mazoezi ya jana alitumia nafasi kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika mchezo wa awali dhidi ya Nigeria.

“Tunafahamu umuhimu wa kushinda mchezo wa kesho (leo), ni mechi ambayo itafufua matumaini ya kwenda ‘World Cup’ ndiyo sababu kila mmoja wetu kambini anaimba wimbo wa ‘Do or Die’,” alisema Mirambo.

Kocha huyo alisema alizungumza na kila mchezaji anachotakiwa kufanya ili kutimiza ndoto ya kucheza Kombe la dunia.

Mirambo alisema miongoni mwa mbinu watakazotumia ni kucheza soka ya nguvu na kumiliki eneo la kiungo ili kudhibiti kasi ya Uganda.

Akizungumzia nafasi ya Serengeti Boys, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali Mstaafu, Idd Kipingu alisema kikubwa ni vijana kujengwa kisaikolojia na kurudishwa mchezoni kwa sababu Uganda wanafungika.

“Kilichopo ni vijana kujengwa na kuaminishwa kuwa wana uwezo kitendo cha kufunga mabao manne kwa Nigeria pamoja na kwamba walipoteza mechi ni hatua kubwa na inaashiria timu haiko vibaya,” alisema Kipingu.

Kipingu alisema aina ya wachezaji ambao Serengeti Boys wanacheza nao kwenye Afcon wana uzoefu wa kutosha katika mashindano ya kimataifa kulinganisha na wao, lakini wamepambana, hivyo hata kwa Uganda nafasi ya kushinda ipo.



Chanzo: mwananchi.co.tz