Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serengeti Boys kuanza na Guinea michuano ya Uturuki

44676 Pic+serengeti Serengeti Boys kuanza na Guinea michuano ya Uturuki

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mashirika. Timu ya taifa ya Tanzania kwa vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys itaanza michuano ya mwaliko ya vijana nchini Uturuki kwa kupambana na Guinea kesho.

Timu hiyo iliyoondoka nchini juzi Ijumaa, itaanza kampeni yake hiyo ikiwa ni mechi ya Kundi A lenye pia timu za Australia na wenyeji Uturuki.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na waandaaji wa michuano hiyo, Kundi A litaanza kwa mechi kati ya wenyeji na Australia wakati Tanzania itacheza na Guinea.

Ratiba ya kundi hilo inaonyesha kuwa mechi ya pili itakuwa kati ya Tanzania na Australia mechi itakayochezwa Machi 6 wakati huo Guinea itakuwa na wenyeji Uturuki. Machi 8 Tanzania na wenyeji Uturuki watakuwa wakimaliza huku Australia ikionyesha na Guinea.

Kundi B mchezo wa kwanza utakuwa Uganda na Cameroon wakati Belarus itacheza na Morocco. Machi 6 Uganda itashuka tena na Morocco na Cameroon itakwaana na Belarus. Mechi za mwisho, Uganda itakutana na Belarus na Morocco dhidi ya Cameroon.

Wakati Serengeti Boys ikitua Antalya, Uturuki mapema jana, Australia iliwasili ikiwa na wachezaji 20, wachezaji 13 wanacheza Hyundai A-League watano wako klabu mbalimbali Ulaya wakati wawili wanatoka Ligi Kuu ya New South Wales.

Mataifa mengine yanayoshiriki michuano hiyo ni; Cameroon, Uganda, Morocco na Belarus zilizo Kundi B wakati Kundi C kuna timu za Senegal, Nigeria, Angola na Montenegro. Kocha wa Australia, Trevor Morgan, aliipongeza Uefa kwa kuipa mechi za majaribio dhidi ya Uturuki, Tanzania na Guinea. “Hii itasaidia kuwafanya wachezaji wetu kuwa na ladha nyingine tofauti.”

Akizungumzia mashindano hayo, Mkuu wa Vyama vya Soka na Uhusiano wa

Kimataifa wa Uefa, Eva Pasquier, alisema: “Huu ni mpango wa Uefa Assist wenye lengo la kugawana uzoefu kwa timu wanachama wa Uefa na marafiki wa Uefa.

“Mashindano haya ya Antalya yanatengeneza vijana na kuwaweka katika mazingira ya mashindano, pamoja na kujifunza utamaduni mbalimbali wa mataifa.”

Michuano hiyo ya Antalya inayaandaa mataifa kwa ajili ya Fainali za Afrika zitakazofanyika Tanzania kuanzia Aprili 14 hadi 28 na timu nne zitafuzu fainali za Kombe la Dunia za U-17 zitakazofanyika Peru kuanzia Oktoba 5 hadi 27.

Mpaka sasa Peru, Australia, Japan, Jamhuri ya Korea, Tajikistan, New Zealand na Visiwa vya Solomon zimeshafuzu na sasa wanasubiri timu nne za CAF na nyingine kutoka CONCACAF na CONMEBOL.



Chanzo: mwananchi.co.tz