Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serengeti Boys haitanii, haiachi kitu kabisa

13271 Pic+serengeti TanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kuna mchezaji mmoja tu Serengeti Boys anaitwa, Kelvin John, ukisikia anatajwa akikokota mpira ujue imoo.

Kelvin anayenyumbulika kwa ustadi dimbani, aliifungia Serengeti Boys mabao matatu dhidi ya Rwanda mchezo wa kukamilisha ratiba wa Kundi A uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam wakati timu hiyo ikiibuka na ushindi wa mabao 4-0. Matokeo hayo yameifanya Serengeti Boys kuongoza kundi lake ikiwa na pointi tisa ikifunga mabao 11, ilizifunga Burundi 2-1, Sudan 5-0 kabla ya jana kuiadhibu Rwanda.

Rwanda inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi zake sita, nafasi ya tatu ikishikiliwa na Burundi huku Sudan ikiburuza mkia.

Mchezo wenyewe

Serengeti Boys ililazimika kusubiri hadi dakika ya 23 kushangilia bao la kuongoza lililofungwa na John lililoipeleka mapumziko ikiongoza kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili Serengeti Boys ikiwa chini ya nahodha, Morice Abraham iliendelea kuinyanyasa Rwanda inayonolewa na Rwasamanzi Yves, kwani dakika 73 mchezaji Aeric Niyonsenga alilimwa kadi nyekundu baada ya kumfanyia faulo mbaya, Kelvin John.

Dakika 78 Serengeti Boys ilipata bao la pili likifungwa na Agiri Ngoda aliyetumia vema uzembe kwa kipa wa Rwanda, Pierre Ishimwe aliyeshindwa kuhamisha mpira aliorudishiwa na beki wake na kumbabatiza John na mchezaji huyo alimchambua kipa huyo kisha akapiga krosi fupi kwa Ngoda aliyeujaza wavuni kwa kichwa kuandika bao la pili.

Bao hilo likawafanya Serengeti Boys kuongeza kasi ya mashambulizi na dakika 83, kiungo Pascal Msindo alipiga pasi iliyopita katikati ya mabeki wa Rwanda na Kelvin John akawapita kwa kasi walinzi watatu na kuuweka mpira wavuni kwa ustadi mkubwa huku wakimfukuzia kwa nyuma.

Dakika 90 Kelvin John tena alikamilisha hat-trick yake katika mchezo huo alipofunga bao la nne kwa Serengeti Boys na kuondoka na mpira anaotuzwa mfungaji wa mabao matatu katika mchezo mmoja. Michuano hiyo inaendelea leo kwa pambano kati ya Kenya na Ethiopia wakati Uganda itacheza na Djibouti.

Chanzo: mwananchi.co.tz