MTENDAJI Mkuu wa Yanga, Senzo Mbatha Mazingiza amekiri kuvutiwa na viwango vya wachezaji wapya waliosajiliwa ndani ya timu hiyo huku akikoshwa zaidi na kiwango kilichoonyeshwa na kipa namba moja wa timu hiyo, Diarra Djigui.
Djigui mwenye uraia wa Mali amesajiliwa na klabu hiyo katika dirisha lilopita la usajili ambapo amefanikiwa kudaka katika michezo yote miwili iliyopita ya Yanga iliyocheza ambapo amecheza bila ya kuruhusu bao ‘clean sheet’.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Senzo alisema kuwa, usajili uliofanywa na klabu hiyo ni mzuri na amevutiwa na viwango vilivyoonyeshwa na wachezaji wote wapya huku akiweka wazi kuwa kipa Djigui ndiye aliyemfurahisha zaidi kutokana na aina yake ya udakaji kuwa ni wa kisasa zaidi.
“Wachezaji wote wapya nimewatazama, ni wazuri na watatusaidia sana kufanya vizuri msimu huu. Siwezi kusema ni mchezaji gani ni bora kuliko wote lakini nimevutiwa zaidi na kipa Diarra Djigui.
“Anavyocheza Djigui ni staili ya makipa wengi wa kisasa, anachezesha timu tokea nyuma, yeye ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi nyingi za mbele zinazofika lakini anapanga mabeki wake vizuri jambo ambalo naamini si rahisi kuwapata kipa wa aina yake, hivyo naamini atatusaidia sana,” alisema kiongozi huyo.
MARCO MZUMBE, Dar es Salaam