OFISA Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mbatha, amefunguka kuwa licha ya baadhi ya mapungufu yanayoonekana kwenye kikosi cha timu yao, lakini uongozi wa klabu hiyo una imani kubwa na kocha wao, Nasreddine Nabi, hivyo apewe muda kutengeneza timu bora Afrika.
Licha ya kuanza vizuri msimu huu kwa kutwaa taji la Ngao ya Jamii na kuvuna pointi sita katika michezo miwili ya kwanza ya Ligi Kuu Bara, Yanga imekosolewa kuwa na mapungufu ya kiufundi ikiwemo muunganiko wa timu na utimamu wa mwili.
Akizungumza na Spoti Xtra, Senzo alisema: “Tumefanya usajili wa wachezaji bora msimu huu na tuna malengo ya kufanya mambo makubwa, hasa kwa kuzingatia matarajio ambayo mashabiki wetu wamekuwa nayo kwa kipindi cha misimu minne iliyopita.
“Lakini ni jambo lililowazi kuwa hatupaswi kuwa na presha ya matokeo kwa sasa kwa kuwa idadi ya wachezaji wapya ambao tumewasajili tunahitaji kumpa kocha wetu Nabi muda wa kutosha zaidi ili kutengeneza muunganiko wao, naamini tukifanikiwa hapo na kwa maendeleo tunayoyaona siku baada ya siku bila shaka tutakuwa miongoni mwa timu bora Afrika.”