KOCHA mkuu wa Simba Pablo Franco mjanja sana. Kumbe siku chache zilizopita alijifungia chimbo na kukisoma kikosi cha Red Arrows ambapo aligundua kuwa kipo bora zaidi kwenye eneo la ulinzi na kuamua kuandaa sapraizi ya kupangua ngome yao.
Pablo, ambaye kesho ataiongoza Simba kwa mara ya kwanza kimataifa katika mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Arrows kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ameamua kuandaa sapraizi ambayo itakuwa kama njia mbadala ‘Plan B’ endapo Wazambia hao watashitukia mbinu zake kuu.
Sapraizi hiyo ni winga Duncan Nyoni ambaye hajawahi kuanza kwenye kikosi cha Simba tangu ajiunge nayo msimu huu lakini amekuwa akiingia kutokea benchi na kuonesha kiwango cha hali ya juu.
Kocha Pablo baada ya kuangalia washambuliaji wake wote, ameamua kumfanya Duncan kama sapraizi ili kuwashangaza wazambia. Katika mazoezi ya juzi yaliyofanyika Mo Simba Arena, Pablo aliwapa nafasi wachezaji wote kuonesha uwezo wao kwenye programu tofauti lakini baadae alihamia kwenye matizi ya kufunga ambapo alimpa nafasi kubwa Duncun ya kucheza winga ya kushoto.
Pablo aliugawa Uwanja robo na kuweka magoli huku akipanga timu mbili zilizocheza kama mechi na kuiamuru timu ya kina Duncan kupiga pasi nyingi ndefu na fupi upande wa kushoto alipokuwepo Duncan.
Fundi huyu kutoka Malawi alikuwa akizituliza pasi zile kwa kontro matata na kukimbia na mpira katika eneo lake kwa spidi akiingia kwenye boksi la 18 alipokuwa mara nyingi akipiga pasi mpenyezo na washambuliaji wakiongozwa na Meddie Kagere kufunga.
Wakati mwingine kutokana na chenga zake na maufundi ya kumiliki mpira, Duncan alijikuta akipigwa viatu na mabeki wa Simba kina Henock Inonga na Pascal Wawa ambao walishindwa kumdhibiti kirahisi hivyo kuwa faulo.
Kocha Pablo alikuwa akipuliza Kipyenga kila Duncan alipochezewa faulo lakini aliendelea kumhimiza kufanya vile vile kwani aliamini hiyo ndio ‘Plan B’ yake kesho.
Ujanja wa Pablo haukuishia kwa kumtengeneza Duncan pekee kama, bali aliwaanda kisaikolojia Peter Banda, Hassan Dilunga na Benard Morrison kwenda kukutana na mabeki imara wa Arrows.
Pamoja na Sapraizi hiyo, Pablo huenda kesho akaanza na wachezaji Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein,Onyango, Inonga, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Rally Bwalya, Kagere, Benard Morrison na Hassan Dilunga huku Ducan akitarajiwa kuingia kutokea benchi