Dar es Salaam. Ndoto ya mshambuliaji wa KRC Genk ya Ubelgiji Mbwana Samatta, kucheza soka nchini Hispania, inaweza kutimia katika usajili wa majira ya kiangazi.
Levante inayoshiriki Ligi Kuu Hispania inamuwinda nahodha huyo wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’, ikitaka kumsajili kabla ya dirisha kufungwa majira ya kiangazi.
Akizungumza na mwananchi katika mahojiano maalumu jana, mshambuliaji wa Levante, Roger Marti amesema mshambuliaji huyo wa zamani wa African Lyon na Simba, atafurahia maisha endapo atajiunga na klabu hiyo.
Marti alisema anasikia sifa za Samatta kuwa ni mshambuliaji hodari mwenye uwezo mzuri wa kufunga mabao na amesikia taarifa za Levante kutaka saini yake katika majira ya kiangazi.
Alisema ana uhakika Samatta akijiunga na Levante atacheza kwa kiwango bora na kuipa mafanikio katika mashindano ya Ligi Kuu Hispania.
Levante imeweka mezani bilioni 10 kwa fedha za Tanzania kunasa saini ya Samatta kuziba pengo la Emmanuel Boateng raia wa Ghana aliyepata majeraha.
Marti alisema ingawa anacheza nafasi ya ushambuliaji, atampa ushirikiano Samatta ili kuzoea haraka mazingira ya Hispania.
“Nasikia ni mchezaji mzuri amewahi kushinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ndani kwa Wachezaji wa Afrika, nadhani atafurahia maisha mapya kama atajumuika na sisi,” alisema Roger.
Levante inasaka mshambuliaji mpya baada ya Boateng kupata maumivu ambayo yatamfanya kukosa mechi za awali za msimu ujao.
Timu hiyo msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya 15 ikiwa na pointi 46 na imebakiwa na washambuliaji watatu akiwemo Marti.
Washambuliaji wengine ni Armando Sadiku raia wa Albania na Mhispania David Salgueiro ambao wameshindwa kupata namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza mbele ya Boateng.
Samatta ambaye pia anawaniwa na CSKA Moscow ya Russia, amefunga mabao 26 tangu alipojiunga na KRC Genk akitokea TP Mazembe ya DR Congo.
Msimu uliopita haukuwa mzuri kwa Samatta kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya goti, Boateng ambaye alikuwa akitegemea na Levante alifunga mabao sita ndani ya msimu huo.
Kinara wa mabao kwa Levante msimu uliopita alikuwa ni kiungo Jose Luis Morales aliyefunga mabao 10 huku akitengeneza nafasi nane za mabao.
Roger alifunga mabao matatu na kutengeneza mawili, Jason alifunga bao moja na kutengeneza mawili na Sadiku ambaye alicheza mechi tano pekee alishindwa kufunga bao hata moja.