Dar es Salaam. Serikali imepanga kuisafirisha timu ya taifa la Tanzania ‘Taifa Stars, kupitia ndege yake mpya ya Boeing 787-8 Dreamliner kwa mara ya kwanza kwenda Cape Verde.
Taifa Stars inatarajiwa kusafiri kati ya Oktoba 9 au 10 kuelekea Cape Verde ambako watacheza mchezo wa kuwania tiketi ya Afcon, Oktoba 12 kwa kucheza dhidi ya wenyeji wao mjini Praia.
Akizungumzia upatikanaji wa ndege hiyo, Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dkt Harrison Mwakyembe alisema hizo ni juhudi za Serikali ambayo imezionyesha kuwa wako mstari wa mbele kuiunga mkono Taifa Stars.
"Watasafiri wachezaji wote na viongozi wa timu, lakini pia hii ni nafasi kwa Watanzania wengine kuambatana na timu kwa ajili ya kwenda kuishangilia huko Cape Verde.
"Ndege haitokwenda na abiria wa safari nyingine itabeba wachezaji na mashabiki pekee, nitoe ombi kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi ili waweze kuchangia gharama za safari hiyo," alisema Mwakyembe.
Waziri huyo alisema kuwa gharama hizo kwa Business Class ni Dollar 2000 huku kwa upande wa Economic Class ikiwa ni dollar 1500 za kimarekani.