Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samatta kama Salah Ubelgiji

15176 Pic+samatta TanzaniaWeb

Sun, 2 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Makali ya mshambuliaji wa Mohamed Salah msimu uliopita wa 2017/18 yaliwafanya mashabiki wa Liverpool kumwimbia wimbo kwa mara ya kwanza pindi walipokuwa wakiitandika Manchester City kwa mabao 4-3 kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Anfield.

Salah ambaye msimu uliopita aliibuka kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu England, aliimbiwa wimbo huo kwa kutajwa jina lake ‘Mo Salah, Mo Salah’ na wakaingizia maneno yenye maana ya kuwa anauwezo wa kukimbiza kwenye winga ‘Salah la la la la la la la’ na mwisho wakamtaja kuwa ni mfalme wa Misri.

Wakati mashabiki wa Liverpool wakifanya hivyo kwa Salah, unaambia Wabelgiji nao wamekuja na mpya kwa kuanza kumwimbia wimbo mshambuliaji wa kutegemewa wa Taifa Stars, Mbwana Samatta.

Samatta amekuwa kipenzi cha mashabiki wa KRC Genk kutokana na kiwango anachoendelea kukionyesha msimu huu wa 2018/19 ambapo tayari ameshaifanya timu hiyo kutinga kwenye makundi ya Kombe la Europa Ligi.

Mashabiki hao wamesikika kwenye michezo kadhaa ya hivi karibuni ya KRC Genk ukiwemo ule aliyepachika mabao matatu ‘hat trick’ dhidi ya Bröndby IF wakiimba ‘Samagoal, Samagoal, Sama..Sama goal lalaaaa. (angalia video kupitia mcl digital)

Makali ya Samatta

Nahodha huyo wa Taifa Stars ametumia dakika 7,851 mpaka sasa kuichezea KRC Genk ya Ubelgiji na kujitengenezea utawala wake kwa kufunga mabao 43 na kutengeneza mengine 12 kwenye jumla ya michezo 121 huku akiwa ameonyeshwa kadi za njano mara 10.

Samatta ameweka wazi kuwa tabia ya kucheka na nyavu alianza nayo akiwa Mbagala Market ambako alicheza soka la kueleweka kabla ya kutua African Lyon na Simba alipojipatia umaarufu.

Baada ya Mbagala Market, alihamia African Lyon na baadaye Simba kabla ya kutua TP Mazembe ambako ilimfanya kutwaa tuzo ya mchezaji bora kwa wachezaji wa ndani Afrika.

“Kama mshambuliaji najivua kufunga, kutengeneza huwa ni ziada kwangu lakini kazi yangu ya kwanza ni hiyo. Ukame wa kufunga ni kitu kibaya ambacho kinaweza kumuathiri mshambuliaji yeyote,” alisema Samatta akizungumza na Mwananchi kutoka Ubelgiji.

Mara baada ya Samatta kutua Genk aliitumikia msimu wake wa kwanza wa 2015/16 kwa kufunga mabao matano na kutengeneza lingine moja kwenye michezo 18 za Ligi Kuu Ubelgiji ‘Jupiler Pro Ligi’ aliyocheza na alitumia dakika 905 huku akionyeshwa kadi moja ya njano.

Samatta alifunga bao lake la kwanza KRC Genk, Februari 28 kwenye mchezo dhidi ya Club Brugge, bao hilo liliamua matokeo ya ushindi kwa Genk ambao walishinda kwa mabao 3-2.

Pia Samatta alionyeshwa kadi yake ya kwanza akiwa na Genk kwenye mchezo huo na ilikuwa dakika ya 90 ya mchezo.

Msimu wa 2016/17, Samatta alitumia dakika 4,115 katika jumla ya michezo 59 kufunga mabao 21 huku akionyeshwa kadi za njano mara nne. Kati ya mabao aliyofunga kwenye msimu huo, 14 aliyafunga ya ligi, mawili Beker Cup na matano ya Europa Ligi.

Msimu wa 2017/18, Samatta alitumia dakika 2, 204 kufunga mabao manane katika michezo 35 huku akitengeneza mengine manne na kupata kadi nne za njano.

Kinachodaiwa kuchangia kutokuwa kwenye kiwango bora ndani ya msimu huo ni kuumia kwenye mishipa midogo ya goti lake la mguu wa kulia ambapo ilibidi afanyiwe upasuaji.

Ndani ya msimu huu wa 2018/19, mshambuliaji huyo aliyekuwa akiwaniwa na Levante ya Hispania amefunga jumla ya mabao tisa kwenye michezo tisa, sita kati ya mabao hayo ameyafunga kwenye mechi tano za Europa Ligi na matatu kwenye michezo minne ya Ligi.

Samatta ametumia dakika 627 msimu huu kufunga mabao hayo huku akionyeshwa kadi moja ya njano.

KRC Genk anayoichezea Samatta imepangwa kundi I baada ya kuivusha kwa kufunga mabao sita na timu anayoichezea Pepe, Besiktas ya Uturuki pamoja na Malmo ya Sweden na Sarpsborg ya Norway.

Samatta ambaye amekuwa akitegemewa na Genk kwenye idara ya ushambuliaji atakutana na Pepe kwenye michezo miwili ya makundi, nyumbani na ugenini ambayo itaanza kutimua vumbi, Septemba 20.

Mara baada ya Genk kutupa karata yao ya kwanza, Septemba watacheza tena mchezo wa pili Oktoba 4 huku mingine ikiwa Oktoba 25, Novemba 8, Novemba 29 na mwisho kwenye hatua hiyo ya makundi itakuwa Desemba 13.

Chanzo: mwananchi.co.tz